Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS AAGIZA VIWANDA NA MIGODI INAYOHARIBU MAZINGIRA KUCHUKULIWA HATUA KALI ZA KISHERIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa viwanda na migodi ambayo inafanya shughuli zake za uzalishaji kwa kuharibu mazingira ikiwemo utitirishaji wa kemikali kwa wananchi kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa wananchi na viumbe hai wengine.


Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo tarehe 4-Jun-2017 kijijini Butiama mkoani Mara wakati anahutubia wananchi katika kilele cha siku ya mazingira Duniani.


Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alisema uharibifu wa mazingira ukiachiwa uendee nchini ni hatari kwa usalama wa maisha na viumbe hivyo ni muhimu kwa viongozi katika ngazi zote kuchukua hatua zitakazosaidia kukabiliana na vitendo hivyo kote nchini.


Makamu wa Rais alisisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kwa ushirikiano na jamii kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuokoa mifumo ya ikolojia, uhifadhi wa bioanuai, kudhibiti uchomaji miti kiholela ili kurejesha uoto wa asili ambao umeharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu katika maeneo mengi nchini.


“Kutozingatia hifadhi ya mazingira kunaweza kusababisha kuparaganyika kwa mfumo huo na kufanya maisha yetu na ya vizazi vijavyo kuwa mashakani”. Alisisitiza Makamu wa Rais.


Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alisema katika kuadhimisha siku ya mazingira Dunia viongozi wanapaswa kuchukua hatua za kuelimisha wananchi na kuwahamasisha ili kila mtu ashiriki katika juhudi za kuwa na uchumi unaozingatia hifadhi ya mazingira.


Kuhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa nchini, Makamu wa Rais aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuruhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa bila kiingilio na kusema mpango huo ni mzuri na unatakiwa kufanyika kila mwaka.


Alisema kuwa mkakati huo unalenga kuhamasisha wananchi ili kuwa mahusiano rafiki na mazingira kwa kuzingatia ukweli kwamba jinsi wananchi wanapoona ndipo wanapoamini na kuelewa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.


Alieleza kuwa katika kuadhimisha siku hiyo inapasa jamii kutafakari mchango wa kila sekta na kila mwananchi katika uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira January Makamba alisema Serikali imeamua kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani kijijini Butiama kama hatua ya kuenzi mchango mkubwa uliofanya na baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere katika uhifadhi wa mazingira.


Alisema baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere alifanya kwa vitendo katika kuhifadhi mazingira ambapo alianzisha msitu wake katika eneo la Butiama hivyo wananchi wote ni lazima waige mfano huo katika kulinda na kutunza mazingira.


Kwa upande wa familia na mwalimu Nyerere wameishukuru Serikali kwa kupeleka maadhimisho hayo kijijini Butiama ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kutambua mchango wa baba wa taifa katika uhifadhi wa mazingira nchini.


Kabla ya Kuhutubia katika Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alipanda miti katika msitu wa Mwalimu Nyerere na kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya ajali ya Ndege ya Kivita ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliopo katika msitu wa Muhunda katika kijiji cha Butiama mkoani MARA.


Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Butiama – Mara
4-June-2017.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com