MALI ZA VIGOGO ESCROW ZAKAMATWA



SERIKALI imekamata mali za wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na mwenzake James Rugemalira wanaodaiwa kuhusika na uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuwafikisha mahakamani.

Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)/Pan Africa Power (PAP) na Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Juni 19, mwaka huu na kusomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ziliiambia MTANZANIA jana kuwa Serikali imelazimika kukamata mali zote za wafanyabiashara hao kama hatua ya kuzuia kuuzwa au kuhamishwa umiliki wake wakati wakiendelea kusota rumande.

“Ni jambo la kawaida katika kesi kama hii, huwezi kuacha mali ambazo ndizo kielelezo katika suala hili. Hivyo hatua ya kwanza ni kumkamata mshtakiwa na kisha ni lazima udhibiti mali zake kwani ndiyo kielelezo muhimu kinachobishaniwa katika kesi husika.

“Unaweza ukaiacha mali halafu mshtakiwa huku akiwa yupo ndani bado akaendelea kutoa maelezo na mali kuhamishwa umiliki wake au hata kuuzwa, kwa hali hiyo ndiyo hulazimika kushikilia mali hizo,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Ofisi ya DPP inaelezwa imezuia mali zote za Sethi na Rugemalira kwa kuziweka chini ya ulinzi mkali pamoja na kufunga kwa muda akaunti zao za benki.

MTANZANIA lilimpomtafuta Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga kupata ufafanuzi wa kina wa hatua ya ofisi yake kushikilia mali za Sethi na Rugemalira, hakupatikana na alipopigiwa simu hakupokea.

Mbali na hayo imeelezwa kuwa orodha ya waliopata mgawo wa fedha hizo za Escrow imezidi kuongezeka, wakiwamo vigogo kutoka wizara nyeti, taasisi, viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya kiserikali na tayari baadhi yao wameanza kuhojiwa na Takukuru mapema wiki hii.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa idadi ya waliohojiwa imefika zaidi ya watu 30 hadi sasa.

Miongoni mwa wanaotajwa kuhojiwa na Takukuru wamo baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne na mtoto wa kigogo wa Serikali, ambao inaelezwa kuwa huenda wakafikishwa mahakamani Jumatatu, huku wengine wakiendelea kuhojiwa zaidi.



MAKOSA SITA

Sethi na Rugemalira walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Juni 19, mwaka huu na kusomewa mashtaka sita.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa udanganyifu na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 (Sh bilioni 309.5).

Walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kupelekwa rumande hadi Julai 3 kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, mwaka 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, watuhumiwa walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Imedaiwa kuwa katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, mwaka 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, wakiwa si watumishi wa umma na wakisaidiana na watumishi wa umma, walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la nne, mtuhumiwa Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua si kweli.

Sethi anadaiwa kutoa nyaraka hiyo ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Makampuni, Seka Kasera kwa nia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka jingine, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 makao makuu ya Benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi St. Joseph, kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola za Marekani 22,198,544.60 (Sh bilioni 309.5).

Katika shtaka la kusababisha hasara Serikali, washtakiwa hao wanadaiwa Novemba 29, mwaka 2013 katika Benki ya Stanbic, Tawi la Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya USD 22,198,544.60 (Sh bilioni 309.5).

Baada ya kumaliza kusomewa mashtaka yao, Wakili wa utetezi, Respicius Didas kwa niaba ya mawakili wenzao, aliomba mahakama iwapatie wateja wao dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga vikali hoja hizo na kuiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo.

Akiwasilisha hoja zake, Wakili Kadushi alisema Mahakama ya Kisutu haina mamlaka si tu ya kutoa dhamana, bali hata kusikiliza maombi ya dhamana.

Alisema mahakama pekee yenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mahakama Kuu na ndiyo maana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote wakati wakisomewa mashtaka yao.
Chanzo-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم