Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUGA ZA WANYAMA UNAZOWEZA KUTEMBELEA BURE WIKENDI HII


 
Siku ya Jumatatu ya Juni 5 itakuwa ni maadhimisho ya ‘Siku ya Mazingira Duniani’ ambayo huadhimishwa na mataifa tofauti duniani ikiwa imebeba kauli mbiu ya ‘Kuwaunganisha Watu na Mazingira Asilia.’

Mapema wiki hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mh. January Makamba alitoa taarifa kwa umma kuwa kwa hapa nchini maadhimisho ya siku hiyo kitaifa yatafanyika kijijini Butiama mkoani Mara, mahali alipozaliwa mwasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Nyerere, ikiwa ni kuenzi jitihada zake za kulinda na kuhifadhi mazingira.
Katika kunogesha sherehe hizo Waziri huyo amesema kuwa serikali imetoa ofa kwa wananchi kutembelea hifadhi yoyote ya mbuga ya wanyama bila ya kiingilio chochote kwa siku tatu, kuanzia Ijumaa ya Juni 2 mpaka Jumapili ya Juni 4. Alisema kuwa lengo kubwa ni kuona uwepo wa wanyama na kujifunza kuwa mazingira yanahitaji kulindwa zaidi na zaidi.
Kauli hiyo ya Waziri imekuja siku chache baada ya kampuni inayojihusisha na masuala ya huduma za hoteli mtandaoni barani Afrika, Jumia Travel kuzindua kampeni ya ‘DemocratizeTravel’ inayolenga kuwakomboa waafrika na watanzania kiujumla katika kusafiri na kutalii vivutio mbalimbali nchini huku wao wakirahisisha huduma za malazi na hoteli.


Kampuni hiyo inalenga kuhamasisha na kutoa elimu juu ya dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa wananchi ya kwamba mchakato mzima unaohusisha utalii ni gharama. Katika kulifanikisha hilo kampuni hiyo imedhamiria kuelimisha juu ya vivutio vilivyopo nchini, masuala ya msingi ya kuzingatia wakati wa kusafiri pamoja na kurahisisha gharama za malazi kupitia hoteli za kila hadhi zilizopo kwenye mtandao wao wa travel.jumia.com. 
Baadhi ya changamoto zilizopo ni pamoja na mwamko mdogo wa watanzania kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo karibu na wanayoishi. Wapo baadhi yao hawafahamu kuwa wanaishi na vivutio hivyo na wengine huchukulia mchakato mzima unahusisha gharama kubwa.

Vifuatavyo ni baadhi ya vivutio vya kitalii ambavyo watanzania mahali popote walipo wanaweza kwenda kuvitembelea wikendi hii bure kabisa kwa mujibu wa kauli ya serikali katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.

Kanda ya Kaskazini. Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Mara kwa kiasi kikubwa imebarikiwa kuwa na hali ya hewa nzuri inayowavutia watalii, hifadhi za mbuga za wanyama, maeneo yenye masalia ya kale pamoja na milima ya kuvutia. Vivutio vinavyopatikana huko ni kama vile; Hifadhi za Taifa za Arusha, Mkomazi, Ziwa Manyara, Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Ngorongoro.
Kanda ya Magharibi. Eneo hili inapatikana mikoa kama vile ya Kigoma na Rukwa ambayo nayo haijaachwa nyuma kwa upande wa vivutio vya kitalii. Wananchi wanaoishi katika au karibu na mikoa hii wanaweza kutembelea Hifadhi za Mbuga za Wanyama kama vile; Gombe, Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane na kujionea wanyama wengi hususani sokwe wa kipekee. 

Kanda ya Kusini. Morogoro, Iringa, Mbeya na Ruvuma ni baadhi ya mikoa inayoweza kupatikana katika ukanda huu ambapo kuna hifadhi za kitaifa kama vile; Kitulo, Mikumi, Ruaha na Udzungwa. Mbuga kama vile Mikumi inajulikana kuwa na idadi kubwa ya wanyama kama vile pundamilia, nyati na tembo. 
Kanda ya Mashariki. Ukanda huu kwa kiasi kikubwa umepakana na fukwe ya bahari ya Hindi ambayo inapatikana kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara. Mbali na kuwa na hoteli nyingi zilizojengwa pembezoni mwa fukwe ya bahari hiyo lakini pia mikoa hiyo inavyovivutio vingine lukuki kama vile; Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Mji wa Bagamoyo, Kisiwa cha Kilwa, Mapango ya Amboni na Mikindani. 


Visiwa vya Zanzibar. Hakuna anayeweza kubisha kuwa vivutio mbalimbali vilivyomo visiwani humo hususani fukwe nyingi safi na za kuvutia pamoja na hoteli za kifahari ndivyo huwatoa watu kutoka mataifa mbalimbali duniani kwenda kuzuru. Mbali na visiwa hivi kusifika kuwa na sehemu nzuri za kupumzika bali pia vina utajiri mkubwa wa tamaduni za watu wa mataifa mbalimbali waliopata kuishi humo kama vile Waarabu, Waingereza pamoja na waafrika kwa ujumla. Lakini pia kuna majengo ya kale yaliyojengwa karne nyingi zilizopita ambayo mpaka leo hii bado yapo na vinginevyo vingi. 
Uzuri wa nchi ya Tanzania umebarikiwa kuwa na vivutio vya kila namna karibuni kila mkoa. Hivyo kisingizio cha kutotembelea sehemu fulani kwa sababu ipo mbali kinakuwa hakina mantiki, Jumia Travel inakushauri anza kwanza na vilivyo karibu nawe na fursa hii iliyotolewa na serikali inaweza kuwa ni mwanzo mzuri kwako.

Na Jumia Travel Tanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com