Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MHADHIRI WA CHUO KIKUU CHA DODOMA PROFESA MWAMFUPE ATEULIWA KUWA DIWANI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amemteua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Davis Mwamfupe kuwa diwani katika Manispaa ya Dodoma.


Juzi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alimtaja Profesa Mwamfupe pamoja na wenzake wawili Roze Nitwa (CCM) na Vicent Tibalindwa (Chadema) kuwa waliteuliwa na Waziri kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.


Kunambi alisema Simbachawene aliteua majina sita kwa vyama vya Chadema na CCM ndipo wakayapigia kura likiwamo jina la Mwamfupe aliyetokea CCM.


“Waziri alitumia sheria namba 288 (24) (2d) ya Serikali za mitaa na kanuni za uteuzi za mwaka 2010 sura ya 4 (1) na 5 (1) vinavyompa mamlaka ya kufanya hivyo bila kuulizwa na humteua mtu ambaye ni mkazi wa eneo husika,” alisema Kunambi.


Manispaa ya Dodoma haina Meya baada ya Jaffary Mwanyemba kuondolewa na madiwani Machi mwaka huu kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.


Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alikana madai ya kumwandaa msomi huo wa uchumi katika nafasi ya Umeya ingawa alisema kila mtu mwenye sifa za kuwa diwani ana haki ya kugombea nafasi ya uongozi ikiwamo meya.


Mkurugenzi huyo aliwaondoa hofu waliokuwa wamejenga nyumba zao katika maeneo ambayo hayajapimwa kabla ya kuvunjwa kwa CDA akisema hawatasumbuliwa badala yake watarasimishwa huku akitoa tahadhari kwa wavamizi wa maeneo na viwanja kuwa lazima watavunjiwa.


Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jumanne Ngede alisema baraza la madiwani halina shaka na uteuzi huo na kwamba watapewa ushirikiano katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ikiwamo mchakato wa makao makuu.


Alisema mpango uliopo katika manispaa hiyo ni kujipanga kuwa na ugeni mkubwa ambao umeingia mkoani hapo ikiwemo maofisa wa serikali.


Mmoja wa madiwani ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema mpango wa uteuzi wa msomi huyo unaweza kuwagawa madiwani kwani kuna kila dalili za kuandaliwa kushika kiti hicho huku wengine wakitaka apewe nafasi katika kamati ya uchumi na fedha tu ili akaonyeshe uzoefu wake huko.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com