Mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa ni Mtanzania amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela nchini Uingereza kwa kosa la kurusha katika ukurasa wake wa Facebook, picha za mtu aliyefariki dunia kutokana na moto uliounguza jengo la ghorofa la Mnara wa Grenfell lililopo nchini humo.
Pia, mtu huyo ametakiwa kulipa faini ya Sh579,880 kwa mwathirika wa tukio hilo.
Mtanzania huyo, Omega Mwaikambo (43) alituma video na picha za mwili wa marehemu uliokuwa kwenye begi na baadaye picha nyingine tano zikionyesha uso wa marehemu huyo.
Gazeti la mtandaoni la The Telegraph limeandika kuwa Mwaikambo amekiri makosa ya kutuma mara mbili picha zisizopendeza kwa umma katika mitandao ya kijamii mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster jana.
Mwaikambo ambaye anaishi hatua chache kutoka lilipo jengo la Grenfell akifanya shughuli za upishi, alishuhudia jinsi jengo hilo lilivyoungua moto usiku na alikuwa ni miongoni mwa wapishi waliowapikia chai wafanyakazi wa zimamoto walipokuwa wakizima moto huo.
“Lakini juzi Jumatano asubuhi alipoangalia miili hiyo nje ya nyumba yake alichukua picha kwa kutumia simu yake aina ya iPad na kuzipakia kwenye mtandao wake wa Facebook,” liliandika gazeti hilo.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Tom Little amesema; “Anaishi karibu zaidi na mnara wa Grenfell, kama ambavyo mahakama inajua janga hilo lilitokea Juni 14.”
Akitoa hukumu, Jaji wa mahakama hiyo, Tanweer Ikram amesema; “Dunia nzima imeshtushwa na yaliyotokea hapa kutokana na janga la moto, ni hali ya kutisha isiyostahimilika, wafu ni lazima waheshimiwe.”
Ameongeza; “Ulichokifanya kupakia hizo picha kwenye Facebook ni dhahiri kuwa hujaonyesha heshima kwa waathirika wa tukio hilo, kuonyesha uso wake hadharani ni kosa kubwa na halielezeki.”
Mpaka sasa watu zaidi ya 17 wanadaiwa kufariki dunia kutokana na moto uliounguza jengo hilo refu na maarufu Magharibi mwa Uingereza.