Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemuhukumu mzee wa Baraza wa Mahakama ya Mwanzo ya Mpanda Mjini mkoani Katavi Anna Mlugala 59 kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na kosa la kupokea rushwa ya Tshs 50,000 kutoka kwa mshitakiwa ambae alikuwa na kesi kwenye Mahakama ya Mwanzo ya Mpanda Mjini.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda CHiganga Ntengwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka ulioongozwa na Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU wa mkoa wa Katavi Simon Buchwa .
Awali mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Simon Buchwa alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Anna Mlugala alitenda kosa hilo hapo Mei 21 mwaka 2015 katika eneo la Mtaa wa Makanyagio Manispaa ya Mpanda .
Mshitakiwa siku hiyo anadaiwa kuwa aliomba rushwa ya Tshs 50,000 kutoka kwa Noelia Kakusu ili aweze kumsaidia kesi yake aliyokuwa ameshitakiwa katika Mahakama hiyo ya Mwanzo ya kuharibu mali .
Mwendesha mashtaka Buchwa aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa alikamatwa baada ya Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa kupata taarifa za mshitakiwa kuomba Rushwa kiasi hicho cha fedha .
Alidai kuwa baada ya TAKUKURU kupata taarifa hizo ndipo walipoweza kuandaa mtego na waliweza kufanikiwa kumkamata mshitakiwa akipokea kiasi hicho cha fedha katika eneo lilikuwa jirani la Mahakama hiyo ya Mwanzo ya Mpanda Mjini
Katika utetezi wake mshitakiwa ambae alikuwa na mashahidi watatu alidai kuwa fedha walizomkamata nazo hakuwa amepewa kama rushwa bali alikuwa amepewa ili akamnunulie vifaa vya kujifungula Noelia Kakusu ambae alikuwa ni mjamzito .
Madai hayo yalipingwa vikari na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Buchwa kwa kile alichoeleza kuwa kitendo cha mshitakiwa Anna Mlugala kutoka Mahakamani wakati kesi ikiwa inaendelea na kutoka nje ya Mahakama na kwenda kuchukua fedha kwa Noelia ni ushahidi tosha kuwa mshitakiwa huyo alikuwa amedhamilia kuchukua rushwa hizo ambazo alikamatwa nazo kufuatia mtego uliowekwa na TAKUKURU.
Hakimu Chiganga baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo na pande hizo zote mbili ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne na mshitakiwa watatu aliiambia Mahakama kuwa pasipo shaka yoyote mshitakiwa amepatikana na hatia ya kosa la kifungu cha sheria Namba 15 ya kudhibiti na kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Hivyo Mahakama imemuhukumu Anna Mlugala kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Tshs 500,000 hadi Mahakama ilikuwa imemaliza kazi zake mshitakiwa alikuwa hajalipa faini hiyo.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi
Social Plugin