NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZATAKIWA KUBORESHA MAZINGIRA YA KISERA KATIKA TAFITI ILI WAKULIMA WANUFAIKE NA KILIMO



Mkulima akionyesha hali halisi ya mazao yake baada ya kukumbwa na ugonjwa wa batobato katika mihogo aliyolima

Mtafiti kutoka (COSTECH) Dk. Nicholaus Nyange akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jitihada wanazochkua kama watafiti nchini katika kukabiliana na magonjwa hayo,Pembeni yake ni Dkt Daniel Otunge akimsikiliza na Mkulima.

Watafiti wakiwa katika shamba la mihogo,kushoto ni mkulima wa mihogo hiyo.
****
Imeelezwa kuwa uboreshaji wa mazingira mazuri ya kisera katika tafiti za kisayansi kwa serikali za Afrika Mashariki kutasaidia wakulima kuondokana na changamoto zinazowakabili sasa za magonjwa yanayokabili mazao pamoja na ukame. 

Hayo yamebainishwa na watafiti kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Taasisi ya Teknolojia ya Kilimo Afrika wakati walipotembelea mashamba ya wakulima wa mihogo,mahindi pamoja na pamba katika mkoa wa Mwanza hivi karibuni. 

Walisema serikali za nchi za Afrika Mashariki hususani Kenya,Uganda na Tanzania zinatakiwa kuweka mazingira mazuri ya ki sera hasa katika tafiti mbalimbali za kisayansi ambazo zipo ili kuwafikia wakulima ili waweze kunufaika na kilimo. 

Watafiti hao walisema magonjwa yanayoikumba Tanzania hasa katika zao la mihogo magonjwa ya Batobato kali na Michirizi ya kahawia ni magonjwa ambayo yapo nchi zote tatu. 

“Magonjwa hayo yapo hata Uganda lakini upande wetu ni hatari zaidi kwani yote mawili yanatokea katika mmea mmoja,hivyo naziomba serikali za nchi zote kuangalia namna ya kuweza kuachia mbegu zilizopo zinawafikia wakulima kwa wakati wakati wanasayansi wanaendelea kufanya utafiti wa mbegu bora zitakazo weza kumaliza hilo tatizo kabisa”,alisema Mtafiti kutoka Uganda Philip Chemonge. 

Nao watatifi kutoka Kenya nao walilalamikia ugonjwa huo wa batobato kali pamoja na michirizi ya kahawia katika zao la mihogo. 

“Hali hii ya magonjwa hata Kenya ipo ambapo kama mtaalamu nilijaribu kulima shamba la mihogo ili iwe shamba darasa kwa wakulima lakini shamba lote lilipata ugonjwa huo na kukosa kuonyesha mfano kwa wakulima,hivyo serikali zinatakiwa kuhakikisha tafiti zilizopo zinafikia wakulima kwa kuwa zimeshaonyesha hali ya kukubaliana na magonjwa hayo ili kuepukana na njaa,”alisema Meneja Mpango wa OFAB-Africa katika Teknolojia ya Kilimo Afrika Foundatio Daniel Otunge. 

Naye Mshauri wa Jukwaa la OFAB nchini na Mtafiti kutoka Tume ya sayansi na Teknolojia, Dk. Nicholaus Nyange alisema jitihada watakazochukua sasa kwa ajili ya kupambana na magonjwa ni kuanza kutoa elimu kupitia mashamba darasa watakayopanga ili njia nzuri ya kutumia mbegu zinazovumilia magonjwa hayo ifahamike kwa wakulima. 

“Kuanzia mwezi wa tisa tutachagua wakulima ambapo tutakuwa na mashamba maalum ya mfano katika kufundishia kwa ajili ya aina ya mbegu zilizoonyesha kuvumilia magonjwa hayo ya batobato na michirizi ya kahawia pamoja na mashamba hayo tutakuwa na mashamba kwa ajili ya kuzalisha mbegu hizo ili kuhakikisha mnapata hizo mbegu na msimu ujao wa kilimo basi muanze kulima polepole aina zinazovumilia magonjwa hayo”,alisema Dk. Nyange. 

Hata hivyo bado jitihada zinatakiwa kwa serikali kuweka kanuni za tafiti za kisayansi vizuri ili kumsaidia mkulima katika kupambana na magonjwa ya mazao pamoja na ukame ambao unasababisha njaa katika taifa. 
Na Hellen David-Malunde1 blog Dar es Salaam 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post