Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amempongeza Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kumpongeza Rais John Magufuli kufuatia uamuzi aliouchukua kuhusu mchanga wa madini yanayochimbwa nchini na kampuni ya Acacia.
Ole Sendeka ambaye aliwahi kuwa msemaji wa Chama Cha Mapinduzi, amesema kuwa baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amempongeza Rais, hana budi kumshukuru na kumpongeza pia kwa kufanya hivyo, na kuwaomba wabunge wote bila kujali vyama vyao kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi.
“Nanyi wabunge mkiwa bungeni muungeni mkono Rais wetu Magufuli anavyotetea rasilimali za nchi ili madini yanayochimbwa yaweze kuwanufaisha Watanzania, waweze kupata huduma zao za msingi kupitia madini hayo,” Ole Sendeka anakaririwa na Mwananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Njombe alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza jana kwenye mazishi ya mama yake mzazi yaliyofanyika katika kijiji cha Losokonoi wilayani Simanjiro.
Alimuomba mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya ambaye alihudhuria mazishi hayo, kumfikishia salamu na pongezi hizo kwa Lowassa.
Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake baada ya kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa makontena ya mchanga wa madini yanayoshikiliwa na Serikali katika bandari ya Dar es Salaam, yalipokuwa katika mchakato wa kusafirishwa nje ya nchi na kampuni ya Acacia.