Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Richard Kwitega amekabidhi zawadi za Eid el Fitr kwa mahabusu ya watoto kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema: "Mheshimiwa Rais ametoa zawadi ya Mbuzi dume, mchele kilo 25 na mafuta ya kupikia lita 10. Vitu hivyo vitawasaidia watoto hao katika kusherekea sikukuu hiyo."
Aidha,amewapa salamu za Rais kwa kuwataka wajue mahali pale ni pa muda mfupi tu hivyo wakitoka wanatakiwa wakawe raia wema na wakajitume zaidi katika kazi na wale ambao ni wanafunzi wakakazane zaidi na shule.
Wakitoa shukrani zao watoto hao wamemshukuru sana katibu tawala kwa niaba ya Rais, na wamempongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika kujenga taifa hili na wao wameaidi wakitoka hapo watakuwa raia wema.
Watoto hao wameiomba serikali kuwasaidia katika usikilizwaji wa kesi zao zisichukue mda mrefu sana na hivyo kupelekea wengi wao kukosa masomo yao ya shule.
Mkurugenzi wa kituo hicho Musa Mapua, amesema tokea mwaka huu uanze ni watoto 48 wameshapita katika kituo hicho na kwa sasa wapo watoto 11 tu na wote ni wa kiume.
Amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kituoni hapo ni ukosefu wa gari la kubeba watoto hao pale wanapoitajika kupelekwa mahakamani na ukosefu wa uzio kwa usalama wa watoto hao. Hivyo ameiomba serikali kukisaidia kituo hicho ili watoto hao wawe katika hali ya usalama zaidi.
Kila mwaka Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa zawadi mbalimbali za Eid katika maeneo mengi ya nchi kwa lengo la kushiriki na walengwa katika kusherekea sikukuu mbalimbali za kidini