Ripoti Twaweza: UMAARUFU WA RAIS UMESHUKA KUTOKA ASILIMIA 96 HADI 71

Asilimia 71 ya wananchi wanaukubali utendaji wa Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani. Kiwango hiki kimeshuka kutoka asilimia 96 mwezi Juni 2016.  Viwango vya kukubalika kwa Rais vinatofautiana katika makundi mbalimbali:
  • Asilimia 68 wenye umri chini ya miaka 30 wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 82 wenye umri zaidi ya miaka 50
  • Asilimia 75 ya wananchi wenye elimu ya msingi au chini yake wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 63 ya wale wenye elimu ya sekondari au zaidi
  • Asilimia 75 ya wananchi masikini wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 66 ya wananchi matajiri
Viwango vya kukubalika kwa viongozi wengine navyo pia vimeshuka katika kipindi hicho hicho.
  • Wabunge:  Kukubalika kwa utendaji wa wabunge kumeshuka kutoka asilimia 79 (Juni 2016) hadi asilimia 58 (Aprili 2017).
  • Madiwani: Kukubalika kwa utendaji wa madiwani kumeshuka kutoka asilimia 74 (Juni 2016) hadi asilimia 59 (Aprili 2017).
  • Wenyeviti wa vijiji/mitaa: Kukubalika kwa utendaji wa wenyeviti wa vijiji/mitaa kumeshuka kutoka asilimia 78 (Juni 2016) hadi asilimia 66 (Aprili 2017).
Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Matarajio na matokeo; Vipaumbele, utendaji na siasa nchini Tanzania. 

Utafiti huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. 

Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa mwezi Aprili mwaka 2017 kutoka kwa wahojiwa 1,805 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya).
 
Kukubalika kwa vyama vya siasa kunatoa taswira mchanganyiko. Kukubalika kwa CCM kumeendelea kuimarika, ikiwa ni kati ya asilimia 54 na asilimia 65 kati ya mwaka 2012 na 2017, Baada ya kushuka mwaka 2013 na 2014 ambapo kiwango cha kukubalika kilifikia asilimia 54 kutoka asilimia 65 ya 2012. 

Kukubalika kwa CCM kumeendelea kubaki katika kiwango hicho hicho cha asilimia 62 tangu uchaguzi wa mwaka 2015 na asilimia 63 mwaka 2017. Kukubalika kwa Chadema kumeshuka hadi asilimia 17 mwaka 2017 kutoka asilimia 32 mwaka 2013.
 
CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (asilimia 80), ukilinganisha na asilimia 55 ya vijana. Wanawake (asilimia 68) wanaikubali CCM kuliko wanaume (asilimia 58), maeneo ya vijijini (asilimia 66) kuliko maeneo ya mijini (asilimia 57), na wananchi masikini (asilimia 69) kuliko matajiri (asilimia 53). Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu ya ufundi au elimu ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46.
 
Kukubalika kwa Chadema kwa ujumla unafuata mtiririko tofauti: ni mkubwa miongoni mwa vijana, wanaume, watu matajiri na wenye kiwango kikubwa cha elimu.
 
Ndani ya kipindi cha miaka miwili tu, vipaumbele vya wananchi vimebadilika sana. Mwaka 2015, asilimia 34 ya wananchi walitaja umasikini na uchumi duni kama moja ya vipaumbele vyao vikubwa ikilinganishwa na asilimia 60 waliotaja masuala hayo mwaka 2017. 

Mwaka 2015, ni asilimia 9 waliotaja upungufu wa chakula au njaa kama kipaumbele chao ikilinganishwa na asilimia 57 mwaka 2017.
 
Katika kipindi hicho hicho, wasiwasi wa wananchi juu ya huduma za umma na rushwa umepungua.

Asilimia ya wananchi wanaotaja masuala yafuatayo kuwa miongoni mwa changamoto kuu tatu zinazoikabili nchi:
  • Afya: asilimia 40 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 59 mwaka 2015.
  • Elimu: asilimia 22 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 44 mwaka 2015.
  • Miundombinu: asilimia 21 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 32 mwaka 2015.
  • Huduma ya maji: asilimia 19 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 46 mwaka 2015.
  • Rushwa: asilimia 10 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 28 mwaka 2015.

==>Soma Ripoti yote hapo Chini


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post