Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linamshikilia mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za injili, Rose Muhando akituhumiwa kujipati fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Debora Mgiligimba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema mwimbaji huyo alikamatwa juzi Wilaya ya Ikungi baada ya wadeni wake ambao ni Waumini wa Kanisa la AICT Singida kupata taarifa kuwa yupo wilayani humo.
Inadaiwa kuwa Novemba 3 mwaka jana, mwimbaji huyo alitumiwa fedha na Mwenyekiti wa Kwaya ya Kanisa la AICT Singida, Mashala Japhet Tsh 800,000 ambapo zilitumwa baada ya pande mbili kukubaliana kuwa angekwenda kwenye uzinduzi wa Album ya kwaya na kanisa hilo, hata hivyo hakutokea.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, uzinduzi wa kwaya hiyo ulikuwa ufanyike Novemba 13 mwaka jana, saa 8 mchana katika uwanja wa Namfua Singida.
Novemba 8 mwaka jana, mwimbaji huyo aliomba kutumiwa tena 150,000 kwa ajili ya nauli ya kutoka Dodoma kwenda Singida yeye na wasaidizi wake, fedha ambayo ilitumwa na mawasiliano yakaendelea kufanyika ili kuakikisha kuwa siku ya tukio anakuwepo.
Cha kushangaza, siku ya tukio msanii huyo hakujitokeza na walipata taarifa kuwa yupo Kahama anatoa huduma, walipofanya mahojiano walithibitisha kuwa ni kweli.
Alipofanyiwa mahojiano na Polisi, Rose Muhando alikiri kutenda kosa hilo kwa kutotoa taarifa kwamba hawezi kuja na alieleza si kweli kwamba alikuwa Kahama, bali alikuwa na mgonjwa nyumbani hivyo hakuweza kutoka. Muhando amesema kuwa yupo tayari kurejesha fedha hizo alizotumiwa.