Taasisi ya Kupambana na Kuzuia na Rushwa (TAKUKURU) jana Juni 19, 2017 iliwafikisha mahakamani wafanyabiashara wawili James Rugemalira na Harbinde Seth watuhumiwa wawili wa kesi za ESCROW na IPTL.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam ambapo wamesomewa mashtaka sita yanayowakabili likiwemo la uhujumu uchumi.
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi alidai Mahakamani hapo kuwa kosa la kwanza la kula njama linawakabili washtakiwa wote wawili ambapo inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Octoba 18, 2011 na March 19, 2014 katika maeneo tofauti ya DSM, Kenya, Afrika Kusini na India walikula njama kwa ajili ya kutenda kosa, ambapo walijipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Katika kosa la pili, la kujihusisha na mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida huku shtaka la tatu ni kughushi ambalo wakili Kadushi alieleza kuwa linamkabili Seth ambapo inadaiwa October 10, 2011 katika mtaa wa Ohio, Ilala DSM akiwa na nia ya ulaghai alighushi cheti cha usajili wa makampuni na kuonesha yeye ni Mtanzania.
Aidha katika shtaka la kutoa nyaraka za kughushi ambalo pia linamkabili Seth ambapo anadaiwa alitoa nyaraka za kughushi katika Ofisi ya Msajili wa makampuni kwa nia ya udanganyifu akiwasilisha fomu namba 14 ya usajili wa makampuni ikionesha ni Mtanzania na mkazi wa mtaa wa Mrikau, Masaki Dar.
Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, wakili Kadushi alidai linawakabili washtakiwa wote wawili ambapo kati ya November 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 katika Makao Makuu ya Benki za Stanbic na Benki ya Mkombozi tawi St. Joseph Dar inadaiwa kuwa, kwa ulaghai washtakiwa hao wote wawili walijipatia Dollar 22,198,544.60 sawa na Tsh. 309b.
Wakili Kadushi alidai kuwa, shtaka la sita ni kusababisha hasara ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya November 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dollar za Kimarekani, 22, 198, 544.60 sawa na Tsh. 309, 461,358.27.
Baada ya kuwasomea makosa hayo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu kitu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka, ambapo wakili Kadushi alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kesi kutajwa.
Mahakama hiyo ilisema upelelezi bado unaendelea na haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa watuhumiwa hivyo walirudishwa rumande.
==>Hapo chini kuna hati ya mashtaka 6 yanayowakaliri
Social Plugin