UINGEREZA YAONGEZA MSAADA KATIKA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NCHINI TANZANIA


Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Hassan Mshinda (kulia), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema wiki hii, wakati serikali ya Uingereza ilipotangaza kuongeza ufadhili wake wa zaidi ya shilingi bilioni 28 katika miradi ya uvumbuzi na teknolojia hasa kwa watoto. Katikati ni Kiongozi wa Timu ya Uwekezaji kwa Watu ya Kitengo cha Kimataifa cha Maendeleo cha Uingereza (DFID) Tanzania, Getrude Kihunrwa na Kiongozi wa timu ya Mfuko wa kuendeleza Uvumbuzi unaofanywa na mwanadamu (HDIF), David McGinty. Picha na Hellen David- Malunde1 blog. 
 ******
SERIKALI ya Uingereza kupitia shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa DFID, imetoa msaada wa shilingi milioni 28.6 kwa ajili ya kusaidia uwekezaji kwenye miradi inayolenga kuinua fursa katika ubunifu wa mambo kwa kutumia teknolojia mbalimbali nchini Tanzania.

Mradi huo ambao ni wa tatu kufanyika nchini umejikita katika malezi bora ya watoto na usafi wa mazingira na ni miongoni mwa miradi ambayo inatekelezwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu unaojulikana kama ( HDIF) na utasimamiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH ).

Akizungumza wakati wa uzinduziwa serikali ya Uingereza  Mkurugenzi wa (COSTECH) Dkt. Hassan Mshinda alilishukuru shirika hilo kuongezea fedha hizo kwani zitatoa nafasi nzuri kwa kupata ubunifu wa vitu ambao utaleta maendeleo katika nyanja ya afya pamoja na elimu.

“Tunashukuru kwa kupata fedha hizi tena kwani nchi bado inahitaji sana kupata njia za kibunifu ambazo zitakuwa njia nzuri kwa kuweza kumuelimisha mtoto ili baadae akikua awe na maendeleo mazuri Zaidi”,alisema Dkt. Mshinda.

Aidha Dkt Mshinda alisema kuwa utafiti waliofanya wao unaonyesha kuwa Mtoto akiwa tumboni na hata baada ya kuzaliwa ni rahisi kumfundisha na akashika jambo vizuri na lisimtoke hata akiwa mkubwa.

“Utafiti unaonyesha kuwa ili mtoto afanye vizuri ukubwani maendeleo yake mazuri yanatakiwa kuanza tangu akiwa mdogo kabisa kwani ndiyo wakati ubongo unaanza kukua pamoja na njia zake za fahamu zinakua ambapo kuna uhusiano mkubwa sana mtu anayefanya vizuri kimaisha na namna alivyoweza kulelewa toka akiwa mtoto mchanga”,aliongeza Dkt. Mshinda.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo kinachosimamia masuala ya uwekezaji kutoka DFID,Bi.Getrude Mapunda alisema fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua maendeleo katika sekta hiyo ya elimu pamoja na upande wa mazingira.

“Tumekuwa tukitoa fedha katika mradi huu wa ubunifu tangu mwaka 2014 kwa kushirikiana na COSTECH ambapo hadi sasa tumepata mafanikio makubwa katika miradi iliyopita 36 na awamu hii ya tatu tunajielekeza zaidi katika usafi wa mazingira ,hedhi kwa wasichana pamoja na makuzi ya watoto wadogo kuanzia miaka sifuri hadi miaka 5”,alieleza.

Naye Mwakilishi mkazi wa HDIF, Bw. David MacGinty alisema  kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwenye miradi iliyopita ndiyo maana wameona ipo haja ya kuongeza ufadhili katika awamu hii ya tatu.

HDIF ilizinduliwa Mei 2014 na makamu wa rais mstaafu wa serikali ya awamu ya nne,Dkt. Mohamed Gharib Bilal lengo likiwa ni kuongeza kasi ya maendeleo pamoja na matumizi ya sayansi na teknolojia katika maendeleo.

Na Hellen David-Malunde1 blog 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم