Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam wafanyabiashara James Rugemarila na Harbinder Sethi kwa tuhuma za uhujumu uchumi na makosa mengine yanayofanana na hao.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa muda mrefu wamekuwa wakiulizwa kuhusu kesi ya Escrow hivyo sasa anaamini ni wakati muafaka wa kuwafikisha watuhumiwa hao wawili mahakamani.
Mlowola alisema kuwa taasisi hiyo imefanya uchunguzi wa kutosha kwa muda wote ambao ilikuwa kimya, na hivyo wamefikishwa mahakamani kisutu na baada ya hapo mahakama itafanya taratibu za kuhamishia kesi hiyo katika Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Kabla ya vigogo hawa wawili kufikishwa mahakamani leo, baadhi ya watumishi wa TANESCO tayari walishtakiwa kufuatia tuhuma za kupokea fedha kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.
Social Plugin