SPIKA wa Bunge Job Ndugai kwa kutumia askari amemtoa nje ya Bunge, mbunge wa Kibamba John Mnyika (Chadema) na kumfungia kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda wa wiki moja, baada ya mbunge huyo kukaidi amri ya kiti cha spika kinyume na Kanuni za Bunge.
Pamoja na mbunge huyo, pia wabunge wengine wa Chadema ambao ni mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, hatma yao itajulikana Jumatatu ijayo, baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwajadili.
Sakata hilo, liliibuka wakati mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Aliwataka wabunge wa upinzani, kuweka wazi kuwa wameamua kutomuunga mkono Rais John Magufuli kuhusu suala hilo la makinikia na badala yake wanaunga mkono wezi ambao wamebainishwa na ripoti ya tume ya uchunguzi wa makinikia hayo.
“Nashangaa kuna wabunge hapa wanaibuka eti wanataka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani naye awajibike kama alivyowajibishwa Muhongo (aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo)...”
“...Naomba niwaulize mbona kipindi kile Chadema mlipomfukuza Kafulila, Mbowe hakuwajibika, au mlipofuta uanachama wa Zitto mbona Dk Slaa hakujiuzulu na yeye? Jamani hebu tuweni makini maana siku hizi imekuwa kawaida zinapokuja hoja nzito zinazogusa hawa wafanyabiashara wanatugawa sisi wabunge,” alisisitiza Lusinde.
Alisema kinachoendelea ndani ya Bunge hilo kwa sasa ni Kambi hiyo Rasmi ya upinzani kuishiwa hoja kutokana na utendaji mzuri wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli.
Kutokana na hoja hiyo ya Lusinde, Mnyika aliomba kuhusu utaratibu kwa Spika, na kumueleza Lusinde kuwa hoja ya upinzani si kupinga hatua hiyo ya kuchunguza makinikia, bali ni kuitaka serikali ising’ang’anie eneo hilo dogo la mchanga na badala yake iweke nguvu kwenye wizi mkubwa wa madini ya dhahabu yenyewe unaofanyika migodini.
Hata hivyo, Ndugai alimweleza Mnyika kuwa hakuitumia vyema kanuni ya kuomba utaratibu, kwani alitakiwa ataje kanuni iliyovunjwa na mchangiaji (Lusinde) kisha akiachie kiti kiamue na si kutoa taarifa kama alivyofanya.
Wakati Mnyika anakaa ili kumpisha Lusinde aendelee kuchangia, sauti ya mmoja wa wabunge mwanamke aliyewasha kipaza sauti ilisikika ikimuita Mnyika mwizi, jambo lililomfanya mbunge huyo ahamaki na kuwasha kipaza sauti chake wakati mwenzake akiendelea kuchangia, akitaka aliyeimuita mwizi athibitishe mbele ya Bunge hilo.
Hata hivyo, alikatishwa na Ndugai, aliyemtaarifu kuwa kwa mujibu wa kanuni Spika hutoa nafasi za kusikiliza anayechangia na aliyeomba taarifa, sauti nyingine za nje huwa hazipewi uzito na kumtaka akae ili mjadala uendelee. “Mimi sina masikio zaidi ya mawili, hayo mengine yanayoendelea sina habari nayo, tuendelee.”
Mnyika hakukubali na aliendelea kuwasha kipaza sauti chake, licha ya kwamba kilikuwa kinazimwa na kutaka aliyemwita mwizi achukuliwe hatua, wakati huo wote spika Ndugai alikuwa akimuonya kwa zaidi ya mara tatu, ndipo aliapoamuru askari wamtoe nje.
Hata baada ya askari kuja kumtoa kwa utaratibu, mbunge huyo aliendelea kuwasha kipaza sauti akidai ameonewa na kwamba atakata rufaa, jambo lililomudhi zaidi Spika ambaye aliwataka askari hao kutumia nguvu na kumtoa nje.
Askari hao walianza kumburuza Mnyika hadi nje huku Mdee akienda na kung’ang’ania koti la moja ya askari na kuvutana nao wakati Bulaya akianza kuhamasisha wabunge wote wa upinzani watoke nje kwa kuwafuata kwenye viti vyao, jambo ambalo pia lilimuudhi Spika.
Kitendo hicho kilimfanya mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) kuomba mwongozo wa Spika, endapo kama ni sawa kwa mbunge kuzunguka kwenye viti vya wenzake na kuwalazimisha kutoka nje wakati Bunge linaendelea.
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema Bulaya amekuwa ni mbunge mtukutu na mjeuri kwa muda mrefu na kuiagiza Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kukutana siku za Jumamosi na Jumapili kumjadili mbunge huyo na Jumatatu Bunge likianza litaanza naye.
Baadaye akifafanua kuhusu kilichotokea, Spika Ndugai alieleza kuwa mbunge yeyote anayeomba kuhusu utaratibu, atalazimika kutaja kanuni au sehemu ya kanuni iliyokiukwa na baada ya hapo ataketi mahali pake kusubiri maelekezo na uamuzi wa spika.
”Mtaona tangu mwanzo sikutaka kumbana (Mnyika) kikanuni sababu alikuwa yupo nje kabisa, completely. Mpaka sasa nikiwauliza ni utaratibu upi alikuwa anazungumzia au kanuni ipi katika kanuni zetu zote hizi aliyokuwa anadai imevunjwa, hutaweza kuipata,” alisema.
Alisema jambo kubwa ni kwamba mbunge huyo alileta fujo na kubishana na Spika kwa kiwango ambacho hakiwezi kuvumilika. “Kwa hiyo nimempa adhabu hiyo ya kutokuwepo hapa wiki nzima. Nilimsikia kwa mbali anasema atakata rufaa akate rufaa tunasubiri sana ujuaji huo.”
Aidha alieleza kuwa wakati fujo hizo zikitokea, pia mbunge Bulaya alikuwa anazunguka ndani ya Bunge hilo na kufanya fujo ikiwemo kuwahamasisha wabunge wa upinzani watoke nje.
Aliitaka kamati ya maadili ikutane jana mchana na kuweka utaratibu wa kumuita mbunge huyo keshokutwa aitwe kwenye kikao hicho na kuagiza kusisitiza hati ya mbunge huyo ya kuitwa mbele ya kamati hiyo awe amepatiwa tangu jana.
Akielezea kosa la Mdee, alisema wakati askari wanamtoa nje Mnyika, Mdee alimvamia askari na kuvuta koti la askari, kitendo ambacho kingemchania askari huyo koti lake. Baada ya vurugu hizo, mijadala ya wabunge iliendelea kama kawaida lakini kutoka upande mmoja wa wabunge wa CCM, kwa kuwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani Bungeni walitoka na kumuunga mkono Mnyika na Bulaya.
Mapema katika Bunge la mkutano wa saba linaloendelea Bulaya na Mdee walisamehewa na Kamati ya Maadili kwa makosa tofauti, ikiwemo kudharau Kiti cha Spika na kulidharau Bunge, baada ya kusimama mbele ya kamati hiyo na kuomba radhi makosa waliyotenda.
Katika hatua nyingine, hali ya hewa bungeni jana ilichafuka baada ya baadhi ya wabunge wa CCM akiwemo Spika wa Bunge Job Ndugai, kuwatuhumu baadhi ya wabunge wenzao huenda wamekuwa wakipokea rushwa, pale inapokuwepo mijadala mizito ya Bunge hilo na kuunga mkono upande usio na maslahi na wananchi.
Tuhuma hizo zilianza kuibuliwa tangu mjadala wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka wa fedha 2017/18 ulipoanza ambapo suala la makinikia ndio lililotawala mjadala huo.
Tangu mjadala huo uanze ndani ya Bunge hilo, kumekuwa na mgawanyiko miongoni mwa wabunge ambapo upande wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni umekuwa ukikosoa uamuzi wa Rais John Magufuli kuchunguza makinikia hayo na kupiga marufuku kusafirishwa nje ya nchi, wakati upande wa wabunge wa chama tawala wakiunga mkono hatua hiyo.
Pamoja na tuhuma hizo, katika hali isiyo ya kawaida, wabunge hao wameiomba Ofisi ya Bunge ianzishe utaratibu wa kuwapima wabunge hao ili kuweza kubaini kama wapo wanaotumia dawa za kulevya ikiwemo bangi.
Tuhuma na madai ya baadhi ya wabunge kupewa rushwa ili watetee upande wa wawekezaji kuhusu sakata la makinikia, zilianza chinichini wakati wabunge wa upinzani wakichangia, ambapo wabunge wanaosadikiwa kuwa ni wa CCM wamekuwa wakiwasha vipaza sauti na kudai kuwa upinzani warejeshe imprest.
Hata hivyo, mbunge wa Geita, Joseph Musukuma (CCM), ndiye aliyechochea tuhuma hizo ambaye wakati akichangia mjadala huo juzi jioni, alithibitisha kuwa wapo wabunge waliopewa fedha kwa ajili ya kuisaliti serikali na kutishia kuwataja.
Kabla ya Musukuma kuwasilisha hoja hiyo, mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) jana bungeni wakati akichangia mjadala huo, alirejea hoja ya Musukuma inayodai upinzani wamelipwa fedha na kusisitiza kuwa endapo hiyo ndio hoja ya mbunge huyo basi akapimwe ili ifahamike kama anatumia bangi kwa kuwa alishawahi kuisifia bangi bungeni hapo.
“Mheshimiwa Musukuma aliwahi kusema hapa bungeni anaunga mkono matumizi ya bangi, leo hii anasema upinzani tumelipwa fedha, naomba akachunguzwe ili ifahamike kama kweli anatumia kilevi hiki,” alisema.
Kutokana na hoja hiyo, Musukuma aliomba kutoa taarifa ambapo alisema kuwa ametajwa na kuhusisha na bangi na kumtaka Spika wa Bunge wabunge wote yeye na Waitara wakapimwe kama wanatumia dawa hiyo ya kulevya na taarifa zao ziwasilishwe ndani ya Bunge hilo.
“Lakini hii hoja kuwa kuna watu wamehongwa jana niliisema hapa bungeni na leo naisema tena, ninawafahamu na uthibitisho ninao semeni su niwataje hapa,” alisema Musukuma bila kuwataja na kumuachia Spika aendelee na mjadala.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), alisema anashangazwa na hoja za baadhi ya wabunge ndani ya Bunge hilo, zinazodai kuwa Chadema kimelipiwa ukumbi kwa ajili ya kufanyia mkutano wake mkuu, ndio maana wabunge wake wanatetea wawekezaji.
“Hivi kweli anasimama mtu hapa anadai chama kikubwa chenye wabunge makini kama Chadema eti kimelipiwa ukumbi. Ina maana chama hiki hakina uwezo wa kujilipia chenyewe?” Alihoji Nassari.
Hata hivyo, hoja yake hiyo ilikatishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alisema Bunge hilo linamuunga mkono Dk Magufuli kwa hatua alizochukua kuhusu suala hilo la makanikia kutokana na uzito wake kwa mustakabali wa taifa.
“Hata nyinyi wabunge mnavyofahamu spika hajawahi kutoka kwenda kwenye jambo lolote la mradi ama kukagua lakini kwa hili niliondoka mimi mwenyewe mpaka kule bandarini pamoja na wabunge baadhi. Kwa uzito wake hili jambo ni kubwa sio dogo...”
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) alisema kwa namna Bunge hilo linavyoendelea ni vyema wabunge wote wakapimwe afya zao ili kujua kama wapo wanaotumia dawa za kulevya au bangi.
IMEANDIKWA NA HALIMA MLACHA-HABARILEO DODOMA
Social Plugin