WANANCHI WAASWA KUMLINDA MTOTO,WAEPUKE MILA POTOFU


Mkuu wa wilaya ya Babati mkoani Manyara Raymond Mushi aliwataka wanajamii na kila mzazi kuweka kipaumbele katika kuimarisha ulinzi na fursa sawa kwa watoto ili kujenga jamii unaojali mustakabali wa mtoto.

Akiongea wakati wa madhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika kijiji cha Minjingu wilayani hapa, yaliyoandaliwa na Shirika watoto na maendeleo ya jamii, World Vision Tanzania (WVT) kwa kushirikiana na serikali wilayani Babati, Mushi alisema suala la ulinzi wa mtoto ni la kila mtu.

‘‘Kila mzazi na kila mwanajamii anatakiwa kulipa kipaumbele suala la ulinzi wa mtoto na kuwatengenezea fursa sawa, hili ni jukumu la kwetu sote na ni muhimu kuhakikisha linafanyika kwa kiwango cha juu’’, alisema Mushi.

Alizitaka jamii nyingi ambazo zimekua na utamaduni wa kuendekeza mila potofu zinazo mkandamiza mtoto na kuchochea unyanyasaji wa kijinsia kama ndoa za utotoni kuacha mara moja.

‘‘Acheni kuendekeza tamaduni na mila potofu zinazokwamisha ulinzi na fursa sawa kwa watoto wa kike na wakiume, muachane na ndoa za utotoni na badala yake sasa mtengeneze mazingira yatakayowawezesha watoto kushiriki katika shughuli za kimaendeleo, hii itafungua milango na uwezo wa kuwalinda watoto na kuwatengenezea fursa sawa’’, aliongeza Mushi.

Awali akimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya, Afisa Maendeleo Msaidizi wa WVT Martha Chalamila kwa niaba ya Mratibu wa eneo la Mradi wa Magugu, lilisisitiza juu ya umuhimu wa wazazi kuweka msimamo katika kuimarisha ulinzi na fursa sawa kwa mtoto na kisha kugawa vipepeprushi vilivyobeba ujumbe maalum uliokua na maelezo ya namna gani siku hii inaweza kutumika kumkomboa mtoto wa Afrika.

“Tunaungana na wenzetu wa World Vision Tanzania na serikali katika maeneo mbalimbali nchini kuadhimisha siku hii kwa kueneza ujumbe wa kuwalinda watoto na kuimarisha fursa sawa kwao”,aliongeza Chalamila.

Ujumbe wa kitaifa ya maadhimisho hayo mwaka huu‘‘Maendeleo endelevu 2030, imarisha ulinzi na fursa sawa kwa watoto’’.

Katika wilaya ya Babati mkoani Manyara, maadhimisho ngazi ya wilaya yalifanyika eneo la mradi wa maendeleo Magugu ambapo wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii walijumuika.

Maadhimisho haya ya siku ya mtoto wa Afrika hufanyika tarehe 16 mwezi wa sita kila mwaka mabapo wadau wa sekta mbali mbali za kimaendeleo duniani na wananchi hujumuika kuadhimisha siku hii kwa kukumbuka na kufanya shughulin mbalimbali zinazo ambatana na ujumbe maalumu unaogusa maisha halisi ya mtoto wa Afrika na changamoto zinazomkabili.


Na Alpha Nsemwa - Babati

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم