Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI DODOMA WAHAMASISHWA KUJITOKEZA KWA WINGI SIKU YA MAADHIMISHO YA MTOTO WA AFRIKA


Wananchi wa Mkoa wa Dodoma wameombwa kujitokeza kwa wingi siku ya Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika kila mwaka June 16 ili waweze kusikiliza na kutambua umuhimu wa siku ya mtoto wa Afrika.

Hayo yameelezwa na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya siku ya mtoto wa Afrika Mkoa Bibi Miriam Silas Nteko ambapo amesema maandalizi yanaendelea vizuri kuanzia siku ya uzinduzi,kongamano na Siku ya Kilele cha maadhimisho hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Kongamano Bw. Mathew Gwawu amesema Kongamano litafanyika tarehe June 15  ,2017   Dodoma Mjini  litakalohusisha watoto mbalimbali kutoka Dodoma na nje ya mkoa pamoja na wadau mbalimbali kutoka kwenye mashirika na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali.

Alisema pia kutakuwa na wasemaji kutoka Shirika la Save the Children, Plan International na maafisa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii jinsia Wazee,viongozi na watoto.

Naye Katibu wa Kamati kuu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Bi. Honoratha Rwegasira amesema Maadhimisho hayo kimkoa yatafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kata ya Haneti, lengo kuu likiwa ni kufuata KAULI MBIU iliyopangwa na Wizara inayosema “MAENDELEO ENDELEVU 2030, IMARISHA ULINZI NA FURSA SAWA KWA WATOTO WOTE”.

Aidha amesema siku hiyo ya maadhimisho ni fursa kwa wana Dodoma na Tanzania kwa Ujumla ambapo wataweza kufikisha ujumbe kwa wana jamii nzima, kuimarisha ulinzi na fursa sawa kwa watoto wote.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Bwana Jaruo Karebe amesema maandalizi yanaendelea Vizuri na mpaka sasa wameunda Kamati nne ikiwemo Kamati ya Uzinduzi, Kongamano,Habari ambao ndiyo wanasaidia kueneza Habari katika jamii na Kamati ya Maadhimisho siku ya Kilele na kamati hizo zitaendelea kufanya kazi hadi siku ya mwisho na amesema ratiba kamili itajulikana tarehe 12 June lakini ameeleza kuwa tarehe 14 itakuwa siku ya Uzinduzi, tarehe 15 itakuwa siku ya Kongamano na tarehe 16 ndiyo kilele cha maadhimisho hayo.


Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Chamwino kitengo cha Wanawake na watoto Bi. Rachel Lugeye amesema katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika shughuli zitakazofanyika siku ya kilele cha maadhimisho hayo ni burudani mbalimbali kutoka kwa watoto zikielezea ujumbe wa siku ya mtoto wa afrika,pia watashirikisha wadau ambao wataeleza shughuli wanazofanya zinazohusiana na mtoto pamoja na kutambua kaya maskini ili waweze kupatiwa misaada mbalimbali.

Kwa Upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi Idara ya watoto kutoka Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto Bwana Emmanuel Barton amesema wao kama Wizara wameridhia Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambayo yote inalenga kumpatia mtoto haki zake za msingi na kuna maeneo wanatakiwa kuyatekeleza kwa mfano kukumbuka suala la mauaji ya watoto yaliyotokea Afrika ya Kusini, amesema kama Wizara wataadhimisha siku hiyo kwa kutoa Press Release ambapo Maadhimisho hayo hayatakuwepo kitaifa bali Wizara wamekuja kuungana na ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kuadhimisha siku hiyo ya mtoto wa Afrika kwa Sababu Dodoma ndiyo Makao Makuu ya Nchi.
Na Josephine Charles- Malunde1 blog Dodoma











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com