Waumini wa dini ya kiislamu mkoani Shinyanga, wameonywa kutotenda dhambi katika sikukuu ya Eid El Fitri kwa kufanya mambo ya anasa bali wamche Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema machoni pake na kusheherekea sikukuu kwa amani na utulivu na kuendeleza matendo mema.
Hayo yamesemwa jana na Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya Swala ya Eid El Fitr iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba mjini Shinyanga Siku ya Eid ni siku takatifu hivyo siyo vyema waumini wa dini hiyo wakatumia mwanya huo kufanya dhambi ambayo itawapeleka motoni.
Alisema ni jambo la aibu kwa muumini wa Kiislamu kufanya dhambi katika sikukuu hiyo ya Eid na hata baada ya Eid kwani itamfanya kufutiwa thawabu zake zote alizozipata wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan hivyo kuwataka waepukane na mambo yote ya kishetani.
“Naomba sherehe hii ya Eid mkasalimie na kutoa zawadi kwa wagonjwa walioko mahospitalini, wafungwa, yatima ,wajane, na hata kutembelea makaburi ya wafu na kuwaombea kwa mwenyezi Mungu mahala huko walipo, na siyo kwenda kwenye maeneo ya anasa na kutenda dhambi,”alisema Makusanya.
Naye mstahiki Meya wa manispaa ya Shinyanga Gulaam Hafeez Mukadam, aliwataka waumini wa dini hiyo kusheherekea siku kuu ya Eid na familia zao, ikiwa ni ibada ya kumcha mwenyezi Mungu na siyo kutumia fursa hiyo kwenda kulewa pombe na kufanya mambo ya ajabu huku akiwaasa kuendelea kutenda mambo mema.
Swala ya Eid El Fitr ikiendelea
Social Plugin