WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU WAZEE WENYE UMRI ZAIDI YA MIAKA 60 KUTOZWA KODI ZA MAJENGO


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka maofisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasitoze kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.


“TRA ijipange kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai mosi 2017. Katika kutekeleza jukumu hilo, zingatieni sheria. Tusisikie mnawadai kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama makazi yao,” alisema Majaliwa.


Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa Wilaya ya Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA wilayani humo mkoani Geita. Waziri Mkuu amewataka moafisa hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu.


“Msiende vijijini. Nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za mijini. Piteni kwenye mitaa, muainishe aina zote za nyumba zinazostahili kulipiwa kodi. Mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha wananchi kulipia kodi hizo,” alisema huku akishangiliwa.


Pia aliwataka wananchi wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia. 


“Ukipewa risiti uiangalie kama ina kiwango halisi cha fedha uliyotoa.Kuna watu wachache wasio waaminifu wanaamua kukupa risiti, lakini imeandikwa bei ndogo kuliko ile uliyolipia, ukitoa laki moja anakupa risiti ya shilingi elfu kumi,” alieleza.


Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana na ulikamilika Juni 12, mwaka huu.


“Ujenzi wa jengo hili umegharimu Sh bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya walipakodi wa Chato kutoka watu 150 mwaka 2010/11 hadi kufikia watu 600 mwaka 2016/17,” alieleza.


Pia alisema wamejenga ofisi hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA ambako ni umbali wa zaidi kilometa 120.


Alisema hivi karibuni watakamilisha ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara, Iringa ikiwemo kujenga ofisi kwenye mikoa mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe na Manyara. “Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa mpya wa kikodi wa Kahama,” alieleza.


Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru. Alisema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya Sh trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم