WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema anaungana na Rais John Magufuli kwa asilimia 100 kukemea mimba kwa wanafunzi na ushoga na kusisitiza kuwa taasisi zinazopigia kampeni masuala hayo, zitafutiwa usajili wao nchini.
Akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Mama wa Yesu, Parokia ya Kisasa mjini hapa jana, Mwigulu alisema suala la mimba kwa wanafunzi na ushoga ni mambo yanayokwenda kinyume cha maadili. Mwigulu alisema taasisi na asasi za kiraia zinazotetea mambo hayo kwa kivuli cha haki, zitafute kazi nyingine za kufanya na kuwa kinyume chake zitafutiwa usajili wao.
“Wanaotaka haki za ushoga wakatafute nchi yao inayoruhusu mambo hayo basi wakakee huko, kama ni taasisi imesajili katika nchi yetu tukaigundua inafanya kampeni ya ushoga, nitazifutia usajili wao,” alieleza Mwigulu na kuongeza: “Na kama ni raia wa Tanzania anaendesha kampeni hizi tutamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, na kama ni raia wa kigeni amekuja kwenye nchi yetu kuendesha haki hizi, tutampa ari ya kuondoka katika nchi yetu na hatapata fursa ya kuchomoa chaja katika soketi.”
Alisema baada ya Rais kutoa tamko hilo na yeye kama idara ya utekelezaji, atalitekeleza ipasavyo. “Aliyosema Rais ni maagizo na si ajenda ya mjadala, na kwenye hilo hatukusanyi ushauri wala maoni, huo ndio msimamo wa serikali, hakuna ushoga, hakuna mimba kwa wanafunzi,” alifafanua waziri huyo ambaye moja ya majukumu ya wizara yake ni kusajili taasisi za kijamii.
“Kwa vile Watanzania tunapenda mijadala, hata hili suala tunalifanya kama la mjadala, na wengine wanasema hivyo na kupigia kampeni za mimba kwa wanafunzi ni waumini sijui wanasoma vitabu gani. “Kwa imani yangu na maandiko yanzuia mimba nje ya ndoa, na yote yanazuia ndoa za utotoni. Waumini wenzetu wanaotaka mimba zihalalishwe wanasoma maandiko gani? Wengine ni akina mama, sijui hayo malezi tunayotaka yaruhusiwe,” Alihoji Mwigulu.
“Mimi namuunga mkono Rais kwa asilimia zote mia. Na niwaombe wote tunasoma vitabu vya Mungu mstari kwa mstari tuunge mkono ukweli huo, ni ukweli kwenye imani sheria na hata busara na utamaduni wetu.” Alisema serikali imetoa haki kwa kila mtoto na ndio maana inatoa elimu msingi bure kwa wanafunzi zote, ilihali kila mtoto apate. Mtoto atakayeamua kuiacha haki hiyo kwa kufanya mambo mengine asipeleke lawama kwa serikali,” aliongeza.
Alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa dini kwa kazi wanayofanya ya kuliombea Taifa na kumuombea Rais kwa sababu ndio msingi wa amani ya Taifa. Alitolea mfano wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambao ulikuwa na taharuki kubwa, lakini juhudi za watu wa Mungu na viongozi wa dini kuomba ndizo zilizofanya ushe kwa amani. “Uchaguzi wa mwaka juzi ulikuwa na taharuki sana, ingawa kuna wengine walioana kama siasa zimetulia sana.
Lakini sisi tuliozunguka kwenye kampeni tuliona hali ilivyokuwa, na kuna wengi walikuwa wanasema ‘Tanzania wanajifanya wana amani hebu tuone mwaka huu.’ “Kiubinadamu na kiserikali maandalizi yalifanyika, kwa sababu ninyi mlipewa uwezo wa kuzungumza na Mungu moja kwa moja, mlipiga magoti, mkaimaliza kazi ile, na uchaguzi ukapita salama, na ulikuwa na utulivu kuliko chaguzi zingine. Hakuna hata mambo ya machozi wala maji ya washawasha yaliyotumika,” alieleza.
Kuhusu kuendelea kumuombea Rais Magufuli, Mwigulu alisema: “Endeleeni kumuombea rais, sisi tunaopata fursa ya kukaa naye karibu tunaiona nia yake iliyo njema, na tunaiona kweli iliyo ndani yake na tunaona anavyojitahidi kwa kiwango kikubwa kutembea katika kweli hiyo. Kweli Mungu amsaidie ili nchi yetu iweze kuwa na maendeleo. Anasema kuwa kuna baadhi ya watu wanaoona maamuzi na hatua zinazochukuliwa na rais ni kuwa amekuwa mkali sana.
“Hivi ni nani akiona uovu hawi mkali? Ni lini mapepo yakakemewa kwa upole? Shetani anakemewa kwa ukali tena kwa mamlaka. Hata Yesu alipotoa pepo alikemea kwa ukali na hata alipoingia Yerusalemu na kukuta uharibifu katika nyumba ya Mungu alikemea kwa ukali. “Rais ana taarifa nyingi na zinapokuwa si njema, kwa kiongozi lazima zinamkasirisha. Kwanza ingeshangaza sana kama anaona uovu akachekelea, hilo lingekuwa la kustaajabisha.
Sio kuoana uovu akakemea likawa jambo la kustaajabisha. Haya anayoyachukua ameanza tu, bado ana mengi ya kuchukua hatua. Hivyo tumuombe ili Mungu amtie nguvu,” alieleza. Alisema jambo zuri kwa Rais Magufuli ni kuwa anapotetea rasilimali za nchi anatetea kwa maslahi ya Watanzania na taifa kwa ujumla.
“Akijenga reli, sio kwamba ataihamishia kwake, au amejenga mabweni basi atapangisha, ila haya anayafanya kwa maslahi kwa faida ya Watanzania,” aliongeza. Alisema hata Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere ambaye amekuwa akitolewa mfano hakuwa na sifa ya kuchekelea uovu, ambayo pia ni sifa ya Mungu pia.
IMEANDIKWA NA ANASTAZIA ANYIMIKE-HABARILEO DODOMA
Social Plugin