Chama cha ACT-Wazalendo kimemtaka Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kujiuzulu kwa kushindwa kuwapelekea wakulima wa korosho pembejeo kama alivyoahidi.
Akizungumza na Waandishi wa habari, jana Julai 30, 2017 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT, Ado Shaibu alisema Serikali iliahidi kuwapa wakulima wa korosho dawa ya kuua wadudu sulpher bure ili waongeze uzalishaji, hivyo chama hicho kinaitaka serikali kutimiza wajibu wake kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo na kama haiwezi kufanya hivyo itangaze taarifa halisi za upatikanaji wa pembejeo hizo kwa wakulima.
”Sisi kama chama cha siasa kwa kuzingatia falsafa ya chama chetu cha siasa ni maendeleo tunaendelea kusisitiza kuwa serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa pembejeo kwa wakulima hawa wa korosho nchini, kuhakikisha kuwa pembejeo husika zinapatikana kwa bei ambayo watanzania wanaimudu na zinapatikana kwa wakati.
"Ni muhimu tukumbuke kuwa unapohujumu zao la korosho unawahujumu wakulima zaidi ya 50,000 wanaojishughulisha na kilimo hicho,” alisema na kuongeza.
“Serikali itoe taarifa za uhakika mapema kuhsu upatikanaji wa pembejeo badala ya kutoa taarifa za hadaa. Ni bora ieleze wazi juu ya uwezo wake ili wakulima waweze kujiandaa mapema kwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kununua pembejeo.
"Iwapo serikali itakuwa haina uwezo wa kugawa salfa yote bure kama inavyoonekana ieleze kwa undani kiwango inachoweza kutoa bure na iimarishe mfumo wa pembejeo.”
Pia ameitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wa pembejeo wanaopandisha bei kila siku bila kuangalia maslahi ya wakulima.
“Serikali ifanye uchambuzi wa kina wa mahitaji halisi ya kila mkulima na kuwa na uhakika wa bajeti yake ndipo itangaze kutekeleza mfumo wa salfa ya bure isikurupuke kwa lengo la kutaka sifa
"Seriklai ifanye haraka kutimiza ahadi yake ya kufikisha pembejeo ya bure kwa wakulima wa korosho kwa kuhakikisha pembejeo ya bure kwa wakulima wa korosho kwa kufikisha kiwango kinacholingana na mahitaji yaliyoko,” amesema.