SERIKALI imesema wiki ijayo itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vya afya na zahanati.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alisema hayo jana mjini hapa wakati wa kufungua kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu maadili na uwajibikaji mahali pa kazi. Dk Ndumbaro alisema vibali hivyo vitatolewa wiki ijayo kwa madaktari, wauguzi na maofisa wa mahesabu 535.
“Maofisa hesabu 535 wataajiriwa kwa ajili ya vituo vya afya vya kata na tumeamua kuwa na maofisa wa hesabu katika vituo vyote vya afya, waganga wakuu wa wilaya watangaze nafasi na waanze kushughulikia ukusanyaji mapato kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo ndani ya kata,” alisema Dk Ndumbaro na kuwataka viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu ili kujenga utumishi wa umma wenye uadilifu.
“Wanaoharibu wasihamishwe na kupelekwa maeneo mengine ukifanya hivyo utakuwa unaharibu utumishi wa umma, ufumbuzi ni kuchukua hatua palepale alipo usimuhamishe kwenye kituo,” alisisitiza. Pia alitaka kujengwa kwa utamaduni wa kuwapongeza watumishi wa umma wanaofanya vizuri kwenye maeneo yao ya kazi.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin