Watu wawili wamefariki dunia na wengine 36 wamejeruhiwa baada ya gari la abiria (daladala) kugonga kichwa cha treni katika eneo la Yombo, Temeke jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa kipolisi wa Temeke, Gilles Moroto (pichani) waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea mapema leo asubuhi ni mwanamke mmoja aliyekuwa abiria wa gari hilo aina ya coaster na mwanaume mmoja ambaye ni kondakta.
Kamanda Moroto amesema kuwa kati ya majeruhi 36 wa ajali hiyo, majeruhi wanne wako katika hali mahututi na kwamba wote wamepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Majeruhi wote wanapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Temeke. Miongoni mwa majeruhi hao, wanne wapo katika hali mbaya,” amesema Kamanda Moroto.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamepongeza juhudi za wananchi kwa ushirikiano wao katika kusaidia kuwaokoa majeruhi wa ajali hiyo kwa kuwatoa ndani ya gari.
Social Plugin