MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi leo aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata na kumweka ndani Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima James Mdee kwa madai kuwa kauli yake aliyoitoa jana Jumatatu wakati akiongea na wanahabari ni ya uchochezi na ya kumfedhehesha Rais John Magufuli.
“Nawaagiza polisi, popote alipo Halima Mdee akamatwe na awekwe ndani kwa muda wa saa 48. Haiwezekani Halima Mdee aseme rais ‘afungwe break’, naomba Mbunge huyo akamatwe ili akalisaidie jeshi la polisi kuhusu maneno hayo,” alisema Hapi wakati anaongea na wanahabari akaongeza kwamba kauli hiyo ni ya uchochezi na yenye kulenga wananchi kuondoa imani na viongozi wao.
“Katika wilaya yangu sitakubali kuwa na wanasiasa kutoa kauli ambazo zinaweza kuleta uvunjifu wa amani katika nchi yetu, niwaombe radhi wananchi wote walioguswa kwa kauli hizo zisizo na staha alizozitoa Mdee,” alisema Hapi.
Jana Halima James Mdee alipinga kauli na msimamo wa Rais Magufuli aliyoitoa hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Pwani kuhusu agizo la wanafunzi wanapopata mimba na kujifungua wasiruhusiwe kurudi shule kusoma.
Mdee alipinga msimamo huo huku akimtaka rais afuate sheria na katiba ya nchi inayowaruhusu watoto hao warudi shule baada ya kujifungua.
Pia alitoa kauli kwamba rais ‘afungwe break’, kauli ambayo imekuwa na maswali mengi miongoni mwa wananchi huku ikitafsiriwa kuwa ni ya kichochezi na kumfedhehesha mkuu wa nchi.
Social Plugin