HARBINDER SINGH AOMBA KUPELEKWA HOSPITALINI KUTIBIWA

MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP) ambaye pia ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, Harbinder Singh Sethi anadaiwa kusumbuliwa na uvimbe tumboni na kwamba anahitaji uangalizi wa madaktari.

Akitoa taarifa hiyo jana, Wakili wa mshitakiwa, Alexi Balomi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, hali ya Seth imeendelea kubadilika kwa wiki nne sasa ambapo imezidi kuwa mbaya kwa kuwa hawezi kupata usingizi.

Balomi alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

‘’Kutokana na hali yake kuwa mbaya wiki hii ni ya nne sasa hawezi kupata usingizi hivyo anahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari tumebahatika kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari. Hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika Kusini,’’ alidai Balomi.

Swai alidai nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka kuziwasilisha mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya sheria na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika mahakamani kueleza hali halisi ya ugonjwa husika.

Hata hivyo, Hakimu Shaidi alisema suala la ugonjwa siyo la kufumbiwa macho, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kuelekeza magereza kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya mshitakiwa huyo inakuwa nzuri na ikibidi, wawasiliane na wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuhakikisha mshitakiwa anapohitajika mahakamani anafika kama inavyotakiwa. Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama laa.

IMEANDIKWA NA FRANSISCA EMMANUEL-hABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post