Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro amefunguka na kusema kuwa jeshi la polisi nchini litaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua mbalimbali baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini wenye lengo la kufanya uchochezi.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo siku mbili baada ya jeshi la polisi nchini kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa kutuhumiwa kutoa maneno ya kichochezi.
Aidha Sirro amedai kuwa jeshi hilo litaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria ambazo ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani viongozi wa vyama vya siasa wanaojaribu kujitafutia umaarufu kwa kutoa kauli zenye utata hasa zile zinazolenga kuchochea vurugu jambo linaloweza kusababisha hali ya uvunjifu wa amani ambayo imedumu hapa nchini kwa muda mrefu.
Viongozi wa CHADEMA ndiyo wamekuwa wahanga namba moja kukamatwa na jeshi la polisi nchini kwa tuhuma za kutoa lugha za kuudhi, na uchochezi ambapo kwa mwezi huu wa saba pekee zaidi ya viongozi 10 wamekamatwa na jeshi la polisi kwa makosa mbalimbali.
Social Plugin