Taharuki imewakumba wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (Sia) mkoani Mbeya na wananchi wanaofanya shughuli kando mwa barabara kuu ya Tanzania -Zambia baada ya moto kuwaka ndani ya eneo la uwanja huo.
Moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika ulitokea jana mchana na kaimu meneja wa uwanja huo, Jordan Mchami alisema iliwachukua takriban nusu saa kuuzima.
Alisema moto huo ulianzia katika eneo la barabara kuu ya Tanzania - Zambia umbali wa mita 600 kutoka maeneo yalipo majengo na eneo la kurukia ndege.
“Tumefanikiwa kuuzima, hakuna madhara yoyote katika eneo letu na si sahihi kusema uwanja umeungua. Ifahamike kwamba uwanja huu una eneo kubwa ambalo ni kama vile pori tu. Moto umetokea barabara kuu ya Tanzania -Zambia umbali wa mita 600 hivi hadi tulipo sisi,” alisema baada ya kuenea taarifa katika mitandao ya kijamii na maeneo ya jirani kwamba uwanja huo umewaka moto.
Alipoulizwa kuhusu cha moto huo Mchami alisema ulionekana kuanzia barabarani na walipofuatilia kwa kuwauliza kina mama wanaofanya biashara ndogondogo kando mwa barabara hiyo waliambiwa kuwa waliona lori lililokuwa limeegeshwa eneo ulikoanzia hivyo wanahisi huenda mtu au watu waliokuwa katika gari hilo walirusha kipande cha sigara na kusababisha nyasi kuwaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema kamanda yupo kwenye msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Hata hivyo, taarifa za ofisa mmoja wa polisi aliyekuwapo eneo la tukio ambaye aliomba jina lake lisiandikwe kwa kuwa si msemaji alisema,“Tumefanikiwa kuuzima moto ambao ulienea eneo kubwa. Tunashukuru haukuweza kufika maeneo ya kurukia ndege au kuharibu mali za uwanja huu.”
Uwanja huo umeongeza wigo wa fursa za kibiashara na kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wakazi wa Mbeya, huku ukianza kuunganisha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine duniani.
Kadri siku zinavyokwenda, watu kutoka nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Malawi wamekuwa wakiutumia uwanja huo.
Wageni hao ambao huingia nchini kwa ajili ya shughuli za biashara na utalii, wamezidi kuifungua kibiashara mikoa ya Songwe na Mbeya na kuonyesha ishara chanya kuwa uwanja huo unaelekea kuwa kitovu cha biashara kati ya Tanzania na nchi za kusini mwa Afrika.