Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema watumishi wa umma walioghushi vyeti watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kairuki amesema hayo jana (Julai 11) katika kikao kazi na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Tarafa ya Mbagala.
Alisema wote walioghushi vyeti hawapo kazini na wameshafutwa katika orodha ya malipo ya Serikali.
Waziri alielekeza waajiri kuwafuta wote wasiostahili kuwepo katika orodha ya malipo na wasimsubiri hadi afike katika maeneo yao ya kazi ili kutekeleza agizo hilo.
“Baada ya uhakiki kukamilika, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa walioghushi vyeti kwa kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyopo katika utumishi wa umma,” alisema Kairuki kama alivyokaririwa katika taarifa iliyotolewa na wizara.
Aliwataka waajiri kuhakikisha wanahakiki taarifa za watumishi wapya wanapoajiriwa na wale wanaohamia ili kujiridhisha kama wana vyeti safi.
“Ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha kuwa vyeti vya kila mwajiriwa mpya vinathibitishwa na mamlaka husika kabla ya kumwajiri na hatimaye kumuingiza kwenye orodha za malipo ya mshahara kupitia mfumo wa HCMIS na mifumo mingine ya mishahara ya kitaasisi,” alisema.
Akizungumzia watumishi wa umma walioajiriwa na sifa za darasa la saba, Kairuki alisema endapo aliajiriwa kabla ya Mei 20 mwaka 2004 anastahili kuendelea kuwa katika utumishi wa umma na endapo kajiendeleza abadilishiwe muundo kuendana na sifa za elimu aliyopata.
Alisema endapo mtumishi huyo aliajiriwa baada ya Mei 20 mwaka 2004 anatakiwa kuwa na sifa ya elimu ya kidato cha nne.
Kairuki pia alitoa ufafanuzi wa kazi inayoendelea inayohusu kuoanisha taarifa za watumishi na zile za usajili uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
“Uhakiki huu utaongeza usahihi wa taarifa za watumishi nchini, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa zinazomhusu mtumishi na kutekeleza azma ya Serikali ya kuunganisha mifumo ya kimkakati ya Tehama ili ibadilishane taarifa,” alisema.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar e Salaam, Theresia Mbando alimpongeza Waziri Kairuki kwa kuboresha utumishi wa umma.
Mbando alisema sasa watumishi wa umma waliobaki kazini wameweza kuziba pengo la waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na kuondolewa kazini.