KITIMTIM cha mgogoro unaohusiana na kuvuliwa uanachama kwa wabunge wanane wa viti maalum ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) na kuteuliwa wengine wapya, kimechukua sura nyingine baada ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad, kuibuka na tuhuma nzito, ikiwamo kumshukia Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Juzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza majina manane ya wanachama wa CUF kutoka kambi ya mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba, kutwaa nafasi ya wabunge wanane wa awali aliotangaza kuwavua uanachama.
NEC ilichukua uamuzi huo ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Ndugai kuridhia uamuzi wa Lipumba, ambao ulihusisha kuondolewa kwa wabunge hao wanaomuunga mkono Maalim Seif.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Maalim Seif alisema uongozi halali wa chama hicho haukubaliani na uamuzi uliofanywa na Spika na kuita kuwa ni hujuma za kisiasa.
Akitolea ufafanuzi jambo hilo wakati akitoa maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lililokutana Zanzibar, Maalim Seif aliitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati suala hilo ikiwamo kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Tanzania na Zanzibar.
Alisema kwa kuzingatia hali ya mambo yanavyokwenda nchini, jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuchukua hatua ili kukomesha kile alichokielezea kuwa ni vitendo vya ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi, ukandamizaji wa demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Katibu huyo alisema baraza la chama chao linaunga mkono wito uliotolewa na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, wa kuitaka jumuiya ya kimataifa kuibana Tanzania kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.
“Tunataka jumuiya ya kimataifa kuibana Tanzania kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi na kuitenga kisiasa na kidiplomasia hadi hapo watawala watakapoamua kuheshimu katiba, sheria, misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria,” alisema Maalim Seif.
Akieleza zaidi, Maalim Seif alisema baraza lao kuu la uongozi la taifa halijakutana popote kufanya maamuzi yoyote ya kuwafukuza uanachama wabunge wanane (8) na madiwani wawili wa CUF kama ilivyodaiwa na Lipumba na kikundi chake.
Alisema kwa msingi huo, Baraza Kuu linawataka Watanzania kufahamu kwamba linaendelea kuwatambua wabunge na madiwani hao (waliotangazwa kutimuliwa na Lipumba) kuwa ni wanachama halali wa CUF, na tena ni wanachama wa kuigwa mfano wa nidhamu na maadili.
“Pamoja na matangazo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza kwamba wabunge hao wanane wamepoteza sifa za ubunge kwa hicho kinachoitwa kufukuzwa uanachama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza majina ya wateule wengine wa kujaza nafasi hizo, Baraza Kuu ambalo ndilo lililowateua hapo awali bado linaendelea kuwatambua kuwa wabunge wake halali,” alisema Maalim katika taarifa yake hiyo.
Aidha, alidai Spika Ndugai amepoteza sifa na haiba ya kuongoza Bunge kutokana na uamuzi wake wa haraka katika kuridhia taarifa ya Lipumba na kikundi chake, hasa kwa kudai kuwa amejiridhisha kuwa uamuzi huo umezingatia katiba ya CUF.
Wabunge waliotangazwa kuvuliwa uanachama na kambi ya Lipumba na kisha Spika kuridhia kabla NEC haijawavua ubunge wao kwa kuridhia kuwa wamekosa sifa kwa kutimuliwa kwenye chama chao ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mwasa, Riziki Ngwali, Raisa Mussa, Miza Haji, Hadija Al-Qassmi na Halima Mohamed.
Wabunge wapya wa viti maalum walioidhinishwa na NEC kutwaa nafasi za wanane waliovuliwa uanachama na kambi ya Lipumba ni Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Kiza Mayeye, Zainab Mndolwa, Hindu Mwenda, Sonia Magogo, Afredina Kahigi na Nuru Bafadhili.
Hadi Nipashe ikienda mitamboni jana, siyo Spika wala Lipumba waliopatikana kuzungumzia madai ya Maalim Seif, aliyosema ni taarifa itokanayo na m aamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.
Social Plugin