MAALIM SEIF AMVAA SPIKA JOB NDUGAI

Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba hatua ya Spika kuwavua ubunge , udiwani na kuteua wengine wapya inalenga kudhoofisha kambi ya wabunge wa CUF na Ukawa.

Amesema Watanzania wanapaswa wajikumbushe kwamba hata kama hicho kinachoitwa ‘kuwafukuza uanachama’ wabunge halali wa CUF kingekuwa kiko sawa, hatua kama hiyo hufuata taratibu zote za kisheria na kikanuni za Bunge kujiridhisha kwanza.

“ Spika Job Ndugai anadhani Watanzania ni vichaa wamuamini kuwa alishachukua hatua ya kujiridhisha kuwa wabunge wanane wa Chama cha Wananchi (CUF) wamefukuzwa uanachama kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge. Ndani ya siku moja?” amehoji Maalim.

Amesema Spika amejiridhisha vipi ikiwa hata hakuwasiliana na Katibu Mkuu wa Chama ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za chama na pia kwa nafasi hiyo ndiye katibu wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama?

Amesema yeye kama katibu, alimuandikia Spika Ndugai barua, Jumanne, Julai 25 akimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu.

“Angekuwa na nia ya kweli ya kutaka kujiridhisha si hapo ndipo pangekuwa pa kuanzia kwa kuwepo kile wanasheria wanachokiita shaka inayoweza kuingia akilini yaani ‘reasonable doubt’?’’ amehoji.


Amesema Spika Ndugai aliyapuuza yote hayo kwa sababu ni kinyume na mkakati wa Dola wa kuihujumu CUF na kuua demokrasia Tanzania. Hapo ndipo Spika Job Ndugai alipolifikisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post