Makubwa Haya : MVULANA WA MIAKA 16 AOA BIBI WA MIAKA 70

Wawili hao wanadaiwa kutishia kujiua iwapo wangezuiwa kufunga ndoa

Mvulana mmoja nchini Indonesia amemuoa mwanamke ambaye amefikisha umri wa miaka 70.

Kisa hicho ambacho kimeenda kinyume na utamaduni na sheria pia kiligunduliwa baada ya video ya harusi ya wawili hao kuanza kusambaa mtandaoni.

Bwanaharusi ana miaka 16 na kirasmi bado ni mtoto lakini maafisa wasimamizi wa kijiji waliruhusu harusi hiyo ifanyike baada ya wawili hao kudaiwa kutishia kujiua.

Chini ya sheria za Indonesia, mwanamke anafaa kuza na angalau miaka 16 na mwanamume miaka 19 ndipo mtu aruhusiwe kufunga ndoa.

Vyombo vya habari nchini humo vinasema urafiki kati ya wawili hao ulianza kunawiri mwanamke huyo alipoanza kumtunza mvulana huyo alipoanza kuugua Malaria.

Chifu wa kijiji chao Kusini mwa Sumatra Cik Ani aliambia shirika la habari la AFP kwamba "kwa kuwa mvulana huyo bado hajafikisha umri wa utu uzima, tuliamua harusi hiyo ifanyike faraghani."

Anasema pia kwamba harusi hiyo iliyofanyika tarehe 2 Julai ilifanyika "kuzuia dhambi ya uzinzi" kati ya mvulana huyo kwa jina Selamat, na mke wake sasa ambaye anatambuliwa kwa jina Rohaya.

Taarifa zinasema Rohaya ana umri wa kati ya miaka 71 na 75.

Babake mvulana huyo anadaiwa kufariki dunia miaka kadha iliyopita na mamake aliolewa na mwanamume mwingine.

Rohaya naye hii ni ndoa yake ya tatu na ana watoto kadha kutoka kwa waume zake wawili wa awali, taarifa zinasema.

Yenni Izzi, mwanaharakati wa kituo cha Women Crisis Centre mjini Palembang ambaye hupigana dhidi ya ndoa za utotoni, aliambia BBC kwamba harusi hiyo ni ya ajabu sana.

"Mvulana huyo aliamua kuoa si kwa sababu za kiuchumi au kimwili lakini kwa sababu anashughulikiwa na kupendwa na mwanamke huyo," alisema.

"Hajakomaa vya kutosha, kwa hivyo kuangaziwa hivyo na kupendwa hivyo anafikiri kwamba wao kuishi pamoja ndio suluhu pekee. Na kuishi pamoja kwake ni kuoana."

Maafisa wa serikali wa kanda wameeleza wasiwasi kuhusu kisa hicho, lakini haijabainika iwapo watachukua hatua.

Waziri wa masuala ya kijamii wa Indonesia Khofifah Indar Parawansa amenukuliwa na gazeti la Jakarta Post akisema kwamba ni "vigumu kwao kuoana rasmi hata katika afisi ya kiongozi wa kidini kwa sababu mvulana huyo bado hajatimiza umri wa kuwa mtu mzima".

Gavana wa jimbo la Sumatra Kusini Alex Noerdin ameambia Sriwijaya Post kwamba "si harusi ya kawaida kamwe. Kuna tofauti kubwa sana kwa umri.

"Katika visa vingi, wasichana ndio huolewa wakiwa wadogo. Lakini katika kisa hiki, ni mvulana aliyeolewa na ajuza, siwezi kusema zaidi ya hapo."
Chanzo-BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post