NB-Picha haihusiani na habari hapa chini
***
Ama kweli ule usemi wa siku za mwizi arobaini unatokea katika mazingira usiyoyategemea!! Mwanamke mmoja ambaye ni mke wa mtu mkazi wa Igoma jijini Mwanza amenusrika kutembezewa kichapo na kuwaacha watu midomo wazi baada ya kubainika kuwa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja aliyekuwa anaishi naye kwa mume wake ana baba watatu.
Mwanamke huyo amenusurika kipigo leo asubuhi baada ya kushindwa kubainisha ukweli juu ya uhalali wa mtoto kutoka kwa wanaume wawili aliokuwa anawavuna pesa huku mme anayeishi naye akishangaa kuona misaada mbalimbali wanayopata watoto anaoishi nao kwa madai kuwa wanahudumiwa na wajomba zake.
Inaelezwa kuwa mwanamke huyo anayeishi na mume wake,huku mume wake akiamini kuwa yeye ndiyo baba wa mtoto kati ya watoto wawili anaoishi nao,kumbe mambo ni tofauti kabisa kwani mtoto huyo analelewa na baba wengine wawili na yeye ni wa tatu.
Wanaume hao watatu wanaishi jijini Mwanza,mmoja Igoma,mwingine mfanyabiashara wa Chips katika Chuo Kikuu cha Sauti Mwanza na mwingine anaishi Igogo.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa mwanamke huyo alikuwa anawaambia wanaume hao kila mmoja kwa wakati wake kuwa amezaa naye na hivyo kuhudumia mtoto huyo.
“Huyu mama anaishi na mme wake,alikuwa anamuaga mmewe kuwa anaenda kwa mjomba wake,anaweza kukaa hata wiki moja na anarudi na nguo za mtoto anamwambia mmewe kuwa zimenunuliwa na wajomba zake kumbe zimenunuliwa na mwanaume mwingine”,walieleza mashuhuda wa tukio hilo.
“Anaporudi nyumbani kwa mmewe,huwa hapokei simu za hiyo michepuko mingine huwaambia wasipige simu kuwa anaishi nyumbani wazazi wake hawapendi kumuona anaongea na simu,kumbe yupo kwa mumewe”,waliongeza.
“Kilichotokea leo ni kwamba kaenda kwa mwanamme mwingine mmoja kati ya hao michepuko wake,simu ikawa inaita imeandikwa ‘Baba Watoto’ akawa hapokei,kila ikiita anaikata,baadae akaenda kuoga,ndipo mchepuko ukaamua kuanza kupekua simu kuangalia hiyo namba ni ya nani haswa”,waliisimulia Malunde1 blog.
Hata hivyo inaelezwa kuwa mwanamme huyo baada ya kupekua simu hiyo alibaini kuwa kuna wanaume zaidi ya mmoja wanahudumia mtoto huyo ndipo akahamaki na kuanza kuwapigia simu mmoja baada ya mwingine ili kujua ukweli.
“Kutokana na sintofahamu hiyo wanaume wote watatu akiwemo anayeishi na mwanamke huyo wakakutana na ndipo vurugu ikaanza wakitaka kumpiga mwanamke huyo lakini wananchi waliokuwa eneo la tukio wakamnusuru asipigwe”,walieleza mashuhuda wa tukio hilo.
Wanaume wawili “Michepuko” waliamua kumuomba mwanamme anayeishi na mwanamke huyo aende na mke wake huku mwenye mke akidai lazima akapime DNA ili kubaini kama watoto wote anaoishi nao ni wa kwake au la!.
Wakizungumza eneo la tukio baadhi ya wananchi walisikika wakisema mwanamke huyo ni miongoni mwa wanawake wengi ambao wamekosa uaminifu na kuwa na tamaa ya pesa ndiyo maana siyo kitu cha ajabu kuona mwanamke ana wanaume zaidi ya mmoja na wote hawajuani.
Na Mwandishi wa Malunde1 blog-Mwanza
Social Plugin