Kampuni ya Barrick Gold ya nchini Canada, imesema wiki ijayo timu ya wataalamu wake watakuja nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzao na Serikali kuhusu uendeshaji wa migodi yake.
Tamko hilo limekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kuwa iwapo Barrick inayoimiliki Kampuni ya Acacia itachelewa kuja kufanya mazungumzo ataifunga migodi yao.
Wakati kampuni hiyo ikijiandaa kuja nchini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tayari imepeleka madaia ya Dola za Marekani bilioni 190 ambazo ni sawa na Sh trilioni 424), kwa Kampuni ya Acacia, ikiwa ni malimbikizo ya kodi kutoka mwaka 2000.
Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Financial Post juzi ilisema. “Kampuni ya Barrick Gold kupitia ripoti yake ya robo mwaka imesema itaanza majadiliano na Serikali ya Tanzania wiki ijayo kuhusu marufuku ya kusafirisha nje madini na masuala mengine yaliyoikumba kampuni inayoimiliki ya Acacia.
“Taarifa hiyo ya mazungumzo inakuja baada ya Jumatatu wiki hii Tanzania kuwasilisha bili ya dola bilioni 190 kwa Accacia yenye makao makuu Uingereza.
“Serikali ya Tanzania inaituhumu Acacia, ambayo inamilikiwa na Barrick kwa asilimia 63.9 kudanganya mapato yake ili kukwepa kodi na hivyo kuitaka ilipe malimbikizo pamoja na faini. Acacia imekana tuhuma hizo.
“Tanzania pia iliweka marufuku ya kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) na fedha Machi mwaka huu, hatua ambayo inaweza kuathiri asilimia sita ya uzalishaji wa wakia milioni 5.3 hadi milioni 5.6 ya dhahabu kwa mwaka katika migodi ya Acacia.
“Barrick ilisema inasubiri hadi Acacia itakaporekebisha mwongozo wake wa uzalishaji kabla ya kubadili mwelekeo mzima wa uzalishaji wake kwa mwaka,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema, Barrick yenye makao yake makuu Toronto, Canada iliripoti kuongezeka kwa mapato kufikia Dola bilioni 1.08 robo iliyoishia Juni 30, kutoka dola milioni 138 kwa mwaka mwaka jana.
“Hilo lilichochewa na mafanikio makubwa ya mauzo ya hisa katika mgodi wa Veladero na mradi wa Cerro Casale. Mtiririko wa fedha kwa kipindi hicho ulikuwa dola milioni 43 ukiwa umeshuka kutoka dola milioni 274 kwa kipindi kama hicho mwaka jana kutokana na kiwango cha juu cha kodi, ongezeko la mtaji na ongezeko lililopangwa kwa ajili ya matumizi ya ukuaji wa badaye,” ilisema.
Juni 14 mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Profesa John Thornton na Ikulu ikatoa taarifa kwa umma kwamba, katika mazungumzo hayo, kampuni hiyo imesema ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
Julai 21, 2017 akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Rais Magufuli alisema. “Nitasimamia haki siku zote katika maisha yangu, na niliwaambia nimeanzisha vita hii ya kiuchumi, vita ya kiuchumi ni mbaya sana, wakubwa wale huwa hawafurahi, kuna viongozi wengi tu mliona yaliyowapata ni kwasababu nchi zao zilikuwa na mali.
“Lakini wale wakubwa wakataka kuchezea hizo mali, kwa manufaa yao na siyo kwa manufaa ya wananchi wa pale, walitumia mbinu nyingi za kila aina, lakini Mungu wangu ni mwema na Watanzania ni wema watasimama kwa ajili ya taifa hili.
“Ninayoongea nayajua ni matrilioni ya fedha ambayo yameibiwa, na kwasasa hivi tumewaita waje wafanye mazungumzo, wamekubali lakini wakichelewachelewa nitafunga migodi yote.
“Ni mara 10 migodi hii tukaigawana Watanzania wachimbe wawe wanauza tuwe tunapata kodi, kuliko kuchimbwa na watu wanaojiita wawekezaji halafu hawalipo kodi.
“Walikuwa wanazungumza mle wanachimba dhahabu, madini machache tu, matatu. tumegundua mle kuna madini mengi.
“Tanzania hii ni nchi tajiri, lakini imekuwa ikiibiwa mno, tumechezewa sana, mimi nipo serikalini na mimi ndiye najua siri za serikali, tumechezewa sana kwa kuibiwa sana mali zetu, kwenye dhahabu huku tumeibiwa mno, ukiyajua yale yaliyokuwa yanafanyike mle unaweza ukalia.
“Unaweza ukatamani usiishi, mtu anachimba anapokea anapeleka na anashirikiana na baadhi ya watu tuliowaamini kwenda kulisimamia hili.
“Anasema hapa tunasafirisha mchanga na Watanzania wote tunaamini tunasafirisha mchanga, mbona hawajaja Kibondo kuchukua mchanga wa hapa mbona na penyewe tunao?
“Lakini tunaamini, wanaupeleka kwenye makontena wanapeleka Ulaya na wakisha enda kuusafisha kule ule mchanga unaobaki wala hawaurudishi, ulikuwa ni utapeli wa ajabu, na ni aibu kubwa kuona utapeli huu unafanywa na watu ambao ni wakubwa.
Julai 26 akiwa mkoani Singida, Rais Magufuli tena alisema “Haiingii akilini watu wanakuja wanachukua mali zetu na kuondoka nazo, ifike mahali tuamke, tumeibiwa vya kutosha, nendeni mkachimbe madini, hizo fedha tutagawana sisi, hata kama hatufanyi kazi hizo fedha tutagawana.
“Wapo wachina wanakuja kuchimba barabara hapa nchini, tunashindwaje kuwatumia hawa wakachimbe madini yetu kisha wakatuachia dhahabu yetu halafu wao wakaondoka?
“Mimi ndiye Rais, hakuna anayejua siri za serikali kama mimi na nawaambia mmepata mtu ambaye anazungumza ukweli, ningeweza kunyamaza kwa vingine ninavyoviona, lakini nataka kujenga Tanzania mpya.
“Yale makontena yote ningeweza kuwaambia tugawane mzee, hata kingereza ninajua, ningeweza kuwaambia give me ten percent (asilimia 10).
“Ningejenga mahoteli na kuwa na kampuni nyingi kwani wapo Watanzania wamejenga huko nje lakini nyumba za wazazi wao zimechakaa, mimi nimezaliwa hapa, ninaishi hapa na nitakufa hapa,”alisema Rais Magufuli.
Social Plugin