MBOWE AMSHITAKI MAHAKAMA MKUU WA WILAYA YA HAI KWA KUHARIBU SHAMBA LAKE

Kampuni ya Kilimanjaro Veggies Ltd inayomilikiwa na Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imefungua kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa.

Imefungua kesi hiyo dhidi ya mkuu huyo wa wilaya kwa kuwa ndiye anayedaiwa kushiriki uharibifu wa miundombinu ya shamba la mbogamboga inalolimiliki wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Kesi hiyo ambayo iko chini ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Aishael Sumari, ilifunguliwa Juni 30, mwaka huu na Kampuni ya Uwakili ya D’ Souza& co ya jijini Arusha kwa niaba ya kampuni hiyo.

Kesi hiyo ina mashauri mawili ambayo ni shauri la ardhi namba 20/2017 na maombi madogo namba 51/2017.

Maombi hayo madogo namba 51/2017, yaliletwa kwa hati ya dharura ambapo mdai anaomba zuio la muda liweze kutolewa dhidi ya mdaiwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Hai asiweze kufanya chochote katika eneo la shamba la hekari 2.7 lililopo katika Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kaskazini, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Aidha, katika kesi hiyo, madai ya msingi ni zuio dhidi ya mdaiwa na wafanyakazi au mtu yeyote asiweze kuingilia eneo husika, mdaiwa aombe radhi kwa vitendo alivyovifanya ikiwa ni pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 549.3 kama hasara aliyoipata mlalamikaji.

Mashauri hayo yamepangwa kusikilizwa Julai 13, mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم