Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MFANYABIASHARA YUSUPH MANJI ASOMEWA MASHTAKA AKIWA AMELAZWA HOSPITALI

Mfanyabiashara Yusuf Manji na wenzake watatu jana wamesomewa mashtaka saba katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako mahakama ilihamia jana kwa muda.


Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhamia hospitalini hapo, alikolazwa Manji.


Manji (41) na wenzake, wanadaiwa kukutwa na vitambaa vyenye thamani ya Sh200 milioni, vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Pia, wanadaiwa kukutwa na mihuri.


Wanashtakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Sheria ya Usalama wa Taifa.


Washtakiwa wengine ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43).


Walisomewa mashtaka hayo ndani ya wodi aliyolazwa Manji na wakati yakisomwa, Manji alikuwa amevaa sare za bluu za wagonjwa na alikuwa ameketi kitandani huku mkononi akiwa ametundukiwa dripu.


Wenzake walisimama pembezoni mwa kitanda chake.


Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali, Tulumanywa Majigo, alidai Juni 30 katika eneo la Chang’ombe A wilayani Temeke, Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ zenye thamani ya Sh192.5 milioni na kwamba, mali hiyo ilipatikana kinyume cha sheria.


Katika shtaka la pili, alidai Julai Mosi katika eneo hilo, walikutwa na polisi wakiwa na mabunda manane ya vitambaa hivyo yenye thamani ya Sh44 milioni mali ambayo ilipatikana isivyo halali.


Washtakiwa katika shtaka la tatu wanadaiwa Juni 30 katika eneo hilo, walikutwa na muhuri wenye maandishi Mkuu 121 kikosi cha JWTZ bila kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.


Majigo katika shtaka la nne, anadai Juni 30 eneo la Chang’ombe A, walikutwa wakiwa na muhuri wenye maandishi Kamanda 834KJ Makutupora, Dodoma bila kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.


Shtaka la tano, wanadaiwa Juni 30 katika eneo hilo walikutwa na muhuri wenye maandishi, Commanding Officer 835KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe bila kuwa na uhalali.


Katika shtaka la sita, wanadaiwa Julai Mosi katika eneo hilo walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SU 383 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.


Washtakiwa katika shtaka la saba, wanadaiwa Julai Mosi kwenye eneo hilo walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SM 8573, ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.


Baada ya kusomewa mashtaka, hawakutakiwa kuzungumza chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuwasilisha hati ya kuipa mamlaka mahakama hiyo kuisikiliza.


Pia, upande wa mashtaka uliwasilisha hati kutoka kwa DPP ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa.


Mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Malimi Seni na Emmanuel Safari walipinga hati ya kuzuia dhamana wakiiomba mahakama isiipokee kwa sababu haina mamlaka na kesi hiyo.


Walidai kitendo cha DPP ni matumizi mabaya ya madaraka na hawatendi haki kwa washtakiwa.


Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 19, kwa ajili ya kutajwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com