Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGEJA AMTAKA SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI ASIMAMIE HAKI NA USAWA NDANI YA BUNGE..USPIKA SIYO TAASISI YA MTU BINAFSI



MWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation,taasisi inayoshulikia utawala bora na haki za binadamu Khamis Mgeja amemuomba na kumtaka Spika wa Bunge Job Ndugai kusimamia haki na usawa ndani ya Bunge na pia kuheshimu mihimili mingine.

Mgeja aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga kabla ya kutimkia Chadema,aliyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani Dodoma akifafanua hali ilivyo ndani ya bunge mkoani humo.

Alisema ndani ya Bunge hivi sasa haki na usawa vinaonekana kutetereka na hasa kwani kinachoendelea sasa wabunge wa kambi ya upinzani wanatimuliwa ndani ya Bunge mara kwa mara kwa sababu ambazo msingi wake ni udhaifu na msukumo wa tofauti za itikadi za kisiasa.

Mgeja alisema watanzania wameshindwa kumuelewa spika wa bunge Job Ndugai jinsi anavyoliendesha bunge hivi sasa hasa katika kipindi hiki kwani kauli zake hazifanani na hadhi ya Uspika amekosa uvumilivu wa kuliongoza bunge watanzania wanaona Ndugai si yule waliyemfahamu huko nyuma amebadilika ghafla.

Alisema kauli anazotoa sasa hivi spika Ndugai tunaona imejaa ubabe,jeuri,dharau na kukosa ustahimilivu subira hasa kwa wabunge wa kambi ya upinzani.


Aliongeza hivi juzi akiongoza bunge alitoa kauli na maneno ya kejeli kwa mahakama na wabunge wa upinzani naomba nimnukuu….."Mara mnakimbia huko na kule mnafungua madudu gani hakuna kesi wala nini nasema mimi ndiyo spika mwaka mzima mtu hakanyagi,mwisho wa kumnukuu.


Alisema anamuomba yeye ndiyo kioo akikosa uvumilivu na kujua kuwa anaongoza bunge lenye itikadi tofauti basi litapoteza haki na heshima yake mbele ya umma.

“Namshauri ni vyema akajifunza na mabunge mengine duniani jinsi wanavyotofautiana hoja mpaka kupelekea kurushiana viti mfano nchini Kenya lakini wanapambana kwa hoja mpaka wanakuwa kitu kimoja kwa maslahi ya mataifa yao.

Alifafanua hakuna sababu ya vitisho na hasa kugusa mihimili mingine na kujiapiza kwani kauli hizo zinakinzana haki za binadamu na utawala wa sheria si dhambi mbunge kumshitaki spika,bunge kama hakutendewa haki.

Mgeja alisema kama bunge au spika yuko juu ya katiba na sheria basi ni vyema watanzania na dunia nzima wajue.

Alisema anamuomba spika Ndugai aache kujikosha kwa watanzania kwa kuwafanya hawana akili kuwa yeye na wabunge wa CCM ndiyo wako sahihi kama malaika na atambue huko nyuma yeye na wabunge wa CCM walipitisha sheria mbovu zinazoliumiza taifa.

Alisema sheria walizopitisha hivi sasa zinapelekea rasilimali za nchi kuporwa mchana kweupe na taifa kupoteza matrilioni ya shilingi na watanzania kushindwa kunufaika na rasilimali hizo.


“Sheria hizo zote yeye kama na akiwa naibu spika huko nyuma
alizisimamia sheria hizo mbovu na hivi sasa Ndugai anachofanya ni
kama kukumbuka shuka wakati kumekucha na watanzania walishalizwa”,alisema.

Mgeja alisema anampa ushauri wa bure mtani wangu Ndugai ni vizuri akajifunza na kupata uzoefu kwa spika mkongwe mzee Pius Msekwa jinsi ya uongozi na uvumilivu na wabunge wanaotofautiana kwa hoja.

Aidha alimuomba pia awaombe radhi watanzania kwa sheria mbovu walizopitisha siku za nyuma yeye na wabunge wenzake wa CCM na waombe radhi wabunge wa kambi ya upinzani.

Mgeja alisema spika Ndugai akitaka kulinda heshima yake na watanzania kuendelea kumkumbuka afanye mambo saba ambayo kutoa uhuru wa mijadala bila kujali itikadi na aangalie maslahi mapana ya nchi.

Alisema kingine ni ikilazimu kushitakiwa awe mfano wa kuheshimu sheria na aheshimu kushitakiwa na awaombe radhi watanzania kwa sheria mbovu walizopitisha za madini,gesi na mafuta siku za nyuma yeye na wabunge wa CCM.

Alisema kingine ni awaombe radhi wabunge wa kambi ya upinzani kwa kuwatendea haki na fukuza fukuza mara kwa mara na aheshimu mihimili mingine kama mahakama kwa maamuzi yoyote yatakayotolewa na mahakama.

Aidha alimuomba pia aibane serikali ianzishe muendelezo wa machakato wa katiba mpya na hasa ile rasimu ya Jaji Joseph Warioba iliyosheheni tunu za taifa na kulinda rasilimali za nchi ndiyo mkombozi wa taifa letu.

Mgeja alimtaka spika Ndugai atambue misingi ya demokrasia na ajue uspika ni taasisi ya umma na si taasisi ya mtu binafsi.

Na Hastin Liumba,Dodoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com