MKAPA AMCHAMBUA RAIS MAGUFULI

Mkapa alisema moyo wa kujitoa na kuwatumikia wananchi alionao Rais Magufuli ndiyo chachu iliyomsukuma kumwamini na kumteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kisha waziri kamili.

Rais wa tatu Mkapa aliyasema hayo jana wakati wa sherehe ya makabidhiano ya nyumba 50 za watumishi wa afya kwa mikoa ya Geita, Simiyu na Kagera zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

"Mimi ninawashukuru zaidi nyie kwa kutambua nguvu zake, utawala wake, hali yake, upeo wake, moyo wake wa kujitoa na kutumikia, na ndivyo vilivyonivutia kumteua kuwa naibu waziri hadi kumpa uwaziri kamili," alisema Mkapa.

Alisema mafanikio yanayopatikana sasa katika sekta ya afya ni juhudi za Rais Magufuli hivyo anapaswa kupongezwa kwa asilimia mia moja.

"Kafanya kazi nzuri, na ataendelea kufanya kazi nzuri," alisema Mkapa. "Mafanikio haya yote ni katika sekta moja tu ya afya."
"Inatunza uaminifu wake, mnastahili kutoa kiongozi wa nchi nzima, tumshukuru Mungu kwa kutupa kijana huyu."

Miongoni mwa mafanikio ya Rais Magufuli katika sekta ya afya, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema jana, ni ongezeko kubwa la bajeti ya wizara yake kwa miaka miwili iliyopita na upatikanaji wa dawa kutarajiwa kuwa asilimia 90 na 100 kuanzia mwaka huu wa fedha.

Waziri Ummy ambaye Rais Magufuli alimsifu kwa kuwa mchapakazi hodari, alisema hatua hiyo inatokana na MSD kutiii maagizo ya mkuu wa nchi huyo kuitaka serikali iagize dawa kutoka kwa wazalishaji bila kupitia kwa dalali.

KAMPENI 1995
Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema anamshukuru Mkapa kwa kumpiga kampeni mwaka 1995 wakati anagombea nafasi ya Ubunge wa Chato.

Alisema wakati anagombea Ubunge, Mkapa wakati huo alikuwa anawania nafasi ya Urais na alimnadi kwa wananchi wa Chato kuwa anafaa na hatimaye alichaguliwa.

"Nakumbuka mwaka 1995 ulipokuja ulikuwa umevaa viatu vyekundu... ulisimama pale (akionesha sehemu ya uwanjani) na ukaniita jukwaani, ukanishika mkono na kuniombea kura kwa wananchi wa Chato... asante sana," alisema Rais Magufuli.

Aidha, Magufuli alisema anamshukuru Rais mstaafu wa nne, Jakaya Kikwete kwa kumwamini na kumteu kuwa Waziri katika wizara mbalimbali.

Rais Magufuli aliishukuru Taasisi ya Mkapa Foundation kwa jitihada zake za kujenga nyumba hizo kwa ajili ya watumishi wa afya, na kwamba taasisi zingine ziige mfano huo.

"Mkapa Foundation wameshatoa ajira zaidi ya 900 kwa madaktari, pia wameshajenga nyumba zaidi ya 400," alisema Rais Magufuli. "Hayo ndiyo maendeleo tunayoyataka, siyo zile taasisi zinaopigia debe wanafunzi kuzaa."

Alisema serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka huu kutoka Sh. bilioni 31 hadi Sh. bilioni 200 huku akiwataka wakuu wa mikoa, wilaya na halmashauri kutumia vizuri pesa za kununulia dawa pindi watakapopelekewa.

Kati ya nyumba hizo, 20 zimejengwa katika mikoa ya Geita, nyumba 20 katika mkoa wa Simiyu na nyumba 10 katika mkoa wa Kagera.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم