Bweni la wanafunzi katika shule ya sekondari Bunambiyu iliyopo katika kata ya Bunambiyu wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga limeteketea kwa moto na kuteketeza mali za wanafunzi 26 wa kike waliokuwa wanalala katika bweni hilo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Muliro Jumanne Muliro alisema tukio hilo limetokea Julai 17,2017 majira ya saa mbili asubuhi.
Alisema mwalimu wa shule hiyo Wilfred John (28) alibaini bweni kuungua moto na kuteketeza mali za wanafunzi 26 wa kike waliokuwa wanalala katika bweni hilo.
Kamanda Muliro alisema chanzo cha moto bado hakijafahamika na kwamba thamani ya mali zilizoteketea hazijafahamika na hakuna madhara kwa binadamu.
Wakati huo huo,nyumba ya mfanyabiashara Amani Issa (39) mkazi wa kitongoji cha Mhunze kata ya Mhunze wilayani Kishapu imeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya shilingi milioni 100.
Kamanda Muliro alisema tukio limetokea Julai 17,2017 majira ya saa 10 jioni katika kitongoji hicho cha Mhunze ambapo nyumba iliungua moto na kuteketeza mali zilizokuwemo ndani zenye thamani ya shilingi 100,000,000/=.
Aliongeza kuwa hakuna mtu aliyedhurika na chanzo cha tukio kinachunguzwa.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog