Polisi nchini India wanasema wamemkamata mzee wa miaka 60 ambaye anatuhumiwa kumuua mkewe kwa kumpiga risasi.
Anadaiwa kuchukua hatua hiyo baada ya mkewe kuchelewesha chakula.
Ashok Kumar alifika nyumbani akiwa amelewa chakari Jumamosi usiku na akaanza ugomvi na mkewe, Rupesh Singh, afisa wa ngazi ya juu wa polisi katika mji wa Ghaziabad karibu na Delhi ameambia BBC.
Sunaina, 55, alikimbizwa hospitalini akiwa na jeraha la risasi kichwani, lakini alifariki njiani.
Bw Kumar amekiri mauaji hayo na kusema sasa anajutia kitendo chake, Bw Singh amesema.
"Mwanamume huyo [Kumar] amekuwa akinywa pombe kila siku. Mnamo Jumamosi, alifika nyumbani amelewa na akaanza ugomvi na mkewe. Mkewe alikuwa amekerwa na tabia yake ya ulevi na alitaka wazungumze, lakini naye alitaka chakula mara moja," Singh anasema.
"Alighadhabishwa na kucheleweshwa kwa chakula na akampiga risasi," ameongeza afisa huyo.
Visa vya wanawake kushambuliwa na waume zao hutokea kwa wingi sana nchini India.
Mwaka 2015, kuliripotiwa kisa cha dhuluma nyumbani kila dakika nne.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na serikali, asilimia 54 ya wanaume wanaamini kwamba ni haki mwanamume kumpiga mke wake iwapo atawakosea heshima mashemeji, kuwatelekeza watoto au kutowajibika nyumbani au hata kufanya kosa dogo kama vile kutoweka chumvi ya kutosha au kuweza chumvi kupita kiasi kwenye chakula.
Asilimia 51 ya wanawake pia walikubaliana na hilo
Chanzo-BBC