Mwenyekiti wa Kitongoji cha German, Kijiji Machochwe wilayani hapa Mkoa wa Mara, Ibrahim Magere amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh20,000.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu wa Wilaya ya Serengeti, Amalia Mushi alisema mshtakiwa ametiwa hatiani katika kesi ya jinai namba 37/2017 kufuatia ushahidi uliotolewa upande wa Takukuru kutoacha shaka.
Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Takukuru, Eric Kiwia alidai kuwa mshtakiwa aliomba Sh20,000 kutoka kwa Joseph Rhobi mkazi wa kijiji hicho aliyekamatwa kwa madai kuwa alikuwa akitafutwa na polisi.
Aliendelea kuwa Rhobi mwaka 2012 alikamatwa na askari wa Kituo kidogo cha Polisi Machochwe, lakini alitoroka akiwa amefungwa pingu ambazo baadaye alizisalimisha kwa mtendaji wa kijiji.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Rhobi alihitaji barua ya utambulisho kutoka ofisi ya kijiji, hivyo mwenyekiti huyo alitoa taarifa polisi na mtuhumiwa alikamatwa.
Hata hivyo, Rhobi aliachiwa kwa dhamana hivyo Mwenyekiti wa Kitongoji alimdhamini huku akimdai Sh20,000 kumaliza suala hilo hali iliyosababisha kutoa taarifa Takukuru na kufanikisha kukamatwa.
Mshtakiwa alipelekewa magereza baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh500,000.