Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka mmoja wa wakimbiza mwenge kitaifa ili aukabidhi mwenge huo kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Aggrey Mwanri (wa kwanza kushoto) leo Jumapili Julai 16,2017katika Kijiji cha Sigiri kata ya Sigiri halmashauri ya wilaya ya Nzega -Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akikabidhi mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Aggrey Mwanri.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akitoa hotuba fupi kuhusu mbio za mwenge mkoani Shinyanga wakati akikabidhi mwenge huo kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Aggrey Mwanri.Kulia ni Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka 2017,Amour Hamad Amour.
HOTUBA YA MHE. ZAINAB R. TELACK MKUU WA MKOA WA SHINYANGA WAKATI WA KUKABIDHI MWENGE WA UHURU KWA MHE. AGGREY MWANRI MKUU WA MKOA WA TABORA TAREHE 16 JULAI, 2017
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Ndg. Makatibu Tawala wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora,
Wahe. Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi Mikoa ya Shinyanga na Tabora,
Ndg. Amour Hamad Amour; Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2017 pamoja na wakimbiza Mwenge Kitaifa na Mkoa,
Wahe. Wakuu wa Wilaya za Mikoa ya Shinyanga na Tabora,
Wahe. Wabunge mliopo hapa,
Ndg. Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama,
Wahe. Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya,
Ndg. Makatibu Tawala wa Wilaya,
Ndg. Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa,
Ndg. Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ndg. Viongozi na watendaji wa Taasisi za Serikali na Mashirika Binafsi.
Ndg. Wadau na wakereketwa wa Mwenge wa Uhuru,
Ndg. Wanahabari,
Ndg. Wananchi Wote,
Mabibi na Mabwana
Shinyanga Hoyee! Tabora Hoyee!
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Awali ya yote nachukua fursa hii adhimu, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukimbiza na kufikisha Mwenge wa Uhuru pamoja na wakimbiza Mwenge katika eneo hili wakiwa salama na afya njema. Aidha, niwashukuru pia viongozi, watendaji na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano na kazi nzuri waliyoifanya kwa kipindi chote ambacho Mwenge wa Uhuru ulikuwa ukikagua, kufungua, kuweka mawe ya msingi na kuhamasisha maendeleo mkoani kwetu. Sisi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga tumejifunza mengi kutoka kwa vijana hawa wakimbiza Mwenge wa Uhuru ambao ni shupavu na makini. Ama hakika tumejivunia sana kuwa nao kwa kipindi hiki kifupi. Nawashukuru sana!
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Katika sherehe hii ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru nimeambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Dini, Watumishi wa Serikali ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga, wadau mbalimbali wa maendeleo waliopo ndani ya Mkoa na baadhi ya Wananchi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Napenda kukushukuru wewe, viongozi mbalimbali wa Serikali na wasio wa Serikali na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kuulaki na kuupokea Mwenge wa Uhuru 2017. Hii ni ishara ya utayari wenu katika kuukimbiza Mwenge wa Uhuru ili kuhamasisha maendeleo katika mkoa wako wa Tabora.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Nitumie fursa hii kueleza taarifa fupi ya hali halisi ya Mkoa wa Shinyanga na kwa namna ambavyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo inavyopambana kuleta Maendeleo kwa Wananchi wake:
Ukubwa wa Eneo la Mkoa na Idadi ya Watu:
Mkoa wa Shinyanga una eneo la kilomita za mraba 18,555. Kwa mujibu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa ulikua na watu 1,534,808 lakini Kutokana na ongezeko la asilimia 2.2 kwa sasa Mkoa wa Shinyanga una watu 1,644,331. Kiutawala, Mkoa umegawanyika katika Wilaya tatu (3) za Kahama, Kishapu na Shinyanga. Mkoa una Halmashauri ya Manispaa moja (1) ya Shinyanga, Halmashauri ya Mji moja (1) ya Kahama, Halmashauri za Wilaya nne (4) ambazo ni Kishapu, Msalala, Ushetu na Shinyanga.
Kukuza Uchumi wa Viwanda katika Mkoa Wetu
Mkoa wa Shinyanga umefanya na unaendelea kufanya jitihada kubwa ya kuvutia Wawekezaji wa ndani na wa nje ili kuwekeza katika Mkoa wetu. Wawekezaji hao wamefungua jumla ya viwanda 81 kati ya viwanda hivyo 18 ni viwanda vikubwa, 9 viwanda vya kati na viwanda vidogo 54. Aidha, Mkoa una viwanda 40 vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo. Viwanda hivyo vimegawanyika kwa mchanganuo ufuatao;- Kiwanda cha nyuzi, kiwanda cha kusindika mafuta ya Pamba, kiwanda cha kutengeneza mabati, mabomba, square pipes, plastic materials, n.k, Kiwanda cha kutengeneza Maji ya Chupa, Juisi na Soda, Viwanda mbalimbali vya Kuchambua Pamba, Kiwanda cha Kutengeneza Vifungashio, Viwanda mbalimbali vya Kusindika Mazao ya Kilimo hususan mpunga na mahindi n.k
Aidha, Mkoa umetenga maeneo mbalimbali kwa ajili wawekezaji wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya Nchi. Tunaendelea kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya Viwanda.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Sisi Mkoa wa Shinyanga tulipokea Mwenge wa Uhuru 2017 na wakimbiza Mwenge sita (6) kutoka mkoa wa Simiyu tarehe 10/07/2017. Katika mkoa wetu, Mwenge wa Uhuru umekimbizwa umbali wa kilomita 802 ambapo Msafara huo umeweka mawe ya msingi, umezindua, umefungua na kuona jumla ya Miradi ya Maendeleo 60 Yote ikiwa na thamani ya Shilingi 15,305,964,195.75 kwa mchanganuo ufuatao:
Nguvu za Wananchi Shilingi 136,525,700.00, Halmashauri Shilingi 2,221,288,340.85, Serikali Kuu Shilingi 2,450,926,122.00, Wahisani Shilingi 2,693,767,165.90 na Sekta binafsi Shilingi 7,793,599,867.00.
Hivyo, kiongozi wa mbio za Mwenge umefungua Miradi 18, kuweka mawe ya msingi miradi 9, kuzindua miradi 11, kukabidhi miradi 1 na kuona miradi 21.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Ujumbe Mkuu wa Mwenge wa uhuru mwaka huu ni “Shiriki kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi yetu”
Ujumbe wa kudumu ni;
· Mapambano dhidi ya Rushwa; Timiza wajibu wako; chini ya kauli mbiu “Tuungane kwa pamoja dhidi ya rushwa kwa maendeleo, amani na usalama wa Taifa letu”.
· Mapambano dhidi ya Madawa ya kulevya; chini ya kauli mbiu “tuwajali na tuwasikilize watoto na vijana”.
· Mapambano dhidi ya UKIMWI; chini ya kauli mbiu “Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI; Inawezekana ifikapo mwaka 2030”
· Mapambano dhidi ya Malaria; Wekeza katika maisha ya baadaye; chini ya kauli mbiu “Shiriki kutokomeza Malaria kabisa kwa manufaa ya jamii”
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Rushwa ni adui wa haki, panapo shamiri rushwa ni dhahiri kuwa haki na usawa hutoweka na kutoa fursa kwa kundi la watu wachache kunufaika. Wito wangu kwa viongozi, taasisi na jamii kuungana kwa pamoja kupinga na kutokomeza rushwa. Katika mkoa wa Shinyanga mapambano dhidi ya rushwa yanaendelea kwa kuweka mbinu mbalimbali za kudhibiti utoaji na upokeaji wa rushwa. Elimu kwa watumishi, viongozi, mashirika na jamii inaendelea kutolewa ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Katika mkoa wetu wimbi la matumizi ya madawa ya kulevya siyo la kutisha. Hata hivyo, Mkoa unaendelea na harakati za kuzuia na kupambana na ushamiri huu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo kubaini Wananchi wanaojihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa kuangamiza nguvu kazi ya Taifa hasa kwa vijana, pia kutoa Elimu kwa Wananchi kuhusu athari za matumizi ya madawa ya kulevya kwa njia ya sinema, majarida, vipeperushi na mabango.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa Mikoa yenye ushamiri mkubwa wa maambukizi ya VVU ukilinganisha na kiwango cha maambukizi ya Kitaifa ambayo ni asilimia 5.1, hii ni kutokana na tafiti ya viashiria vya UKIMWI na Malaria ya mwaka 2011 – 2012 (Tanzania HIV and Malaria Indicator Survey-THMIS 2011/2012) ambapo Mkoa ulionekana kuwa na ushamiri wa maambukizi ya VVU kwa asilimia 7.4 (kiwango cha maambukizi kwa wanaume ni asilimia 6.6 na wanawake ni Asilimia 8.1.). Aidha, takwimu za ndani ya Mkoa zilizotokana na huduma zote za upimaji wa VVU kwa mwaka 2015, Mkoa ulikuwa na ushamiri wa maambukizi ya asilimia 4.6.
Juhudi za kukabiliana na janga la UKIMWI katika Mkoa wetu zinaendelea ili tuweze kufikia sifuri tatu, baadhi ya shughuli zinazofanyika kwa sasa ni kutoa Elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na maambukizi, kuwahamasisha kupima afya zao, kuwahudumia Wananchi na Watumishi waliopima na kukutwa na maambukizi, kutoa huduma ya tohara kwa wanaume, huduma za wagonjwa wa majumbani, kuhakikisha hakuna maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua pamoja na huduma ya utambuzi wa maambukizi kwa watoto wachanga.
Wananchi walioitikia na kujitokeza kupima kwa hiari maambukizi ya VVU walikuwa 4,163 ambapo wanaume ni 2,937 na wanawake ni 1,226 Waliogundulika kuwa na maambukizi walikuwa 84 sawa na asilimia 2 ikiwa wanaume ni 53 na wanawake ni 31 .Nitoe pongezi kwa wote waliojitokeza kupima na kujua afya zao na kwamba ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwa mwangalifu na kulinda usalama wa afya za wengine.
Wananchi waliojitokeza kupima kwa malaria walikuwa 426 ambapo wanaume ni 309 na wanawake ni 117 Waliogundulika kuwa na ugonjwa wa malaria ni 26 sawa na asilimia 6.1 ikiwa wanaume ni 17 na wanawake ni 9.
Aidha, kwa wale waliobainika kuwa na maambukizi ya VVU nawashauri wazingatie masharti waliyopewa na wataalam wa afya. Pia, Nitoe wito kwa wote ambao bado hawajapima afya zao wajitokeze kwa wingi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupima, kujua na kupanga namna ya kuboresha afya zao.
Ndg. Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2017,
Kwa niaba ya viongozi na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, napenda kukupongeza wewe binafsi pamoja na vijana wenzako mnaokimbiza Mwenge wa Uhuru. Hakika tumefarijika sana kukutana nanyi kwani ni vijana shupavu, jasiri, wachapakazi, wazalendo na wenye uthubutu mkubwa! Niwashukuru sana kwa kazi kubwa mliyofanya katika kipindi chote mlichokuwa nasi, tulipenda kuendelea kuwa nanyi kwa siku nyingi zaidi, ila kwa kuwa mnatakiwa kuendelea katika Mikoa mingine basi hatuna budi kutoa fursa kwa Mikoa mingine kuendelea kujumuika nanyi katika mbio hizi za mwenge wa uhuru. Tunawatakia afya njema na kuwaombea muweze kumaliza jukumu mlilokabidhiwa kwa usalama, mkipata nafasi karibuni tena Mkoani Shinyanga!!
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Vijana hawa sita (6) ni miongoni mwa watanzania wachache wenye Moyo wa kizalendo waliojitoa kwa dhati kuukimbiza Mwenge wa Uhuru na kueneza ujumbe wake kwa umahiri mkubwa katika hali na mazingira yote. Vijana hawa ambao nitakukabidhi hivi punde, tumewapokea, kuwalea na kuwatunza vizuri sana. Kwa kipidi chote tulicho kaa nao wametupa ushirikiano wa kutosha na sasa tunawaleta kwako wakiwa salama na wenye afya njema.
Baada ya kusema hayo, sasa naomba nikukabidhi wakimbiza Mwenge wa Uhuru wakiongozwa na Ndg. Amour Hamad Amour, kama ifuatavyo;
1. Ndg. Fredrick Joseph Ndahani (Singida)
2. Ndg. Salome Obadia Mwakitalima (Katavi)
3. Ndg. Vatima Yunus Hassan (Kusini Pemba)
4. Ndg. Shukran Islam Msuri (Mjini Magharibi)
5. Ndg. Bahati Mwaniguta Lugodisha (Geita) na
6. Ndg. Amour Hamad Amour kiongozi wa Mbio za Mwenge, 2017 (Kaskazini Unguja)
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Kwa heshima na taadhima leo tarehe 16/07/2017 naomba nikukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2017 ukiwa salama, unang’ara na kumelemeta ili uweze kufanya shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika Mkoa wako wa Tabora.
Mwenyezi Mungu awajalie afya njema na mafanikio katika kutekeleza kazi mlizopanga.
MWENGE WA UHURU HOYEE!
MKOA WA SHINYANGA HOYEE
TABORA HOYEE.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MAKABIDHIANO YA MWENGE,MKOA WA SHINYANGA KWA MKOA WA TABORA
Mwenge wa uhuru ukiwa katika kijiji cha Sigiri kata ya Sigiri Halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora ambapo makabidhiano yamefanyika
Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga wakiwa eneo la tukio baada ya kumaliza mbio za mwenge mkoani Shinyanga,wakijiandaa kukabidhi mwenge huo kwa mkuu wa mkoa wa Tabora.
Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga wakifurahia eneo la tukio
Viongozi wakiendelea kufurahia kwa kumaliza salama mbio za mwenge mkoani Shinyanga.
Wakimbiza mwenge wakipiga ngoma eneo la makabidhiano
Viongozi wa mkoa wa Tabora wakijiandaa kupokea mwenge wa uhuru ili ukimbizwe katika mkoa huo.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akitoa hotuba fupi kuhusu mbio za mwenge mkoani Shinyanga
Wakimbiza mwenge wa uhuru wakiwa eneo la tukio
Viongozi wa mkoa wa Shinyanga wakiwa eneo la makabidhiano
Tunafuatilia kinachoendelea hapa...
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akitoa hotuba fupi kuhusu mbio za mwenge mkoani Shinyanga
Mmoja wa wakimbiza Mwenge akishikana mkono na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2017,Amour Hamad Amour akizungumza eneo la tukio ambapo alisema kati ya miradi yote aliyoipitia mkoani Shinyanga,hakuna mradi alioukataa
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka 2017,Amour Hamad Amour akishikana mkono na mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack.
Mkuu wa mkoa wa Tabora,Aggrey Mwanri akimkaribisha Tabora Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka 2017,Amour Hamad Amour
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka mmoja wa wakimbiza mwenge kitaifa ili aukabidhi mwenge huo kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Aggrey Mwanri (wa kwanza kushoto)
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akikabidhi Mwengewa Uhuru kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Aggrey Mwanri
Zoezi la makabidhiano likiendelea
Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Aggrey Mwanri akisoma taarifa ya miradi ya maendeleo itakayozinduliwa na mwenge wa uhuru mkoani humo
Viongozi wa mkoa wa Tabora wakijiandaa kukimbiza mwenge wa uhuru
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,mheshimiwa Josephine Matiro akiwa na mkuu wa wilaya ya Tabora,mheshimiwa Queen Mlozi wakipiga kumbukumbu
Viongozi wilayani Kahama na Shinyanga wakibadilishana mawazo baada ya zoezi la kukabidhi mwenge wa uhuru kumalizika.
Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog