Mwenyekiti wa (CUF) anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa, Profesa Lipumba amefunguka na kusema kuwa Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ana kesi ya kujibu na kudai yeye kawaponza wabunge nane waliovuliwa uanachama wa CUF.
Profesa Lipumba amesema hayo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na kusema Katibu Mkuu wa (CUF) Mhe. Maalim Seif na yeye ana yake ya kujibu mbele za Kamati ya Maadili na Nidhamu ya CUF.
"Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na kuna wananchama wengine wengi tu ambao pia wana makosa ya kuweza kujibu mbele ya Kamati ya Nidhamu na Maadili katika watu wote hao Katibu Mkuu yumo na yeye ndiye amewaponza hawa wabunge nane wa Viti Maalum ambao wamevuliwa uanachama na ndugu zangu wa Zanzibar na wale wabunge wengine wale msiwe mnasikiliza na kufuata kila anachosema Katibu Mkuu atakuponza kama alivyowaponza wajumbe wa baraza la wawakilishi" alisema Lipumba
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CUF Taifa Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema mpaka sasa wabunge wote nane ambao wanasemakama wamefukuzwa uanachama wameamua kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga maamuzi feki ambayo yamefanywa na Baraza Kuu feki na kuitaka Mahakama itamke kuwa wao ni wanachama halali wa CUF na wabunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini pia Katibu Mkuu amesema kuwa Baraza Kuu halali la CUF litakutana kwa dharura siku ya kesho Ijumaa tarehe 28/07/2017 kujadili mambo mbalimbali ambayo yanaendelea katika chama hicho na kutangaza hatua ambazo zitafuata.