Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) limewavua uanachama wabunge wanane wa chama hicho kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwa ni pamoja na kukisaliti chama hicho.
Akizungumza jana na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, mbali na wabunge hao, baraza hilo pia limewavua uanachama madiwani wawili wa viti maalumu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa makosa kama hayo.
Lipumba amesema wabunge hao waliovuliwa uanachama ni miongoni mwa wabunge kumi waliosusia wito wa kwenda kujieleza juu ya tuhuma zinazowakabili za kula njama na CHADEMA ili kuweza kumuondoa yeye madarakani.
Aidha, Lipumba aliwaambia waandishi wa habari kuwa, taarifa kuhusu uamuzi huo tayari zimeshatumwa kwenda kwenye Ofisi ya Spika wa Bunge na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya hatua zaidi.
Wabunge 10 walioitwa kuhojiwa na chama hicho inadaiwa kuwa ni wale wanaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif.
Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa zilizopo chini ya CUF, wamesema binafsi hawatokuwa tayari kuhojiwa kwani hawamtambui kiongozi huyo.
Social Plugin