Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amembadilikia Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mh Aziz Abood na kumtaka arudishe viwanda mbalimbali ambavyo alibinafsishiwa na serikali kama ameshindwa kuviendesha.
Rais Magufuli amesema hayo leo alipokuwa Morogoro mjini na kuwataka watu waliobinafsishiwa viwanda na serikali mkoani humo na wameshindwa kuviendesha wavirudishe kwa serikali ili serikali iweze kuwapa watu wengine ambao wataweza kuviendesha.
“Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mbali na hilo Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro SACP - Ulrich Onesphory Matei kuhakikisha askari Mgambo hawawasumbuli wafanyabiashara wadogo wadogo na amewataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.
Rais Magufuli wakati akiwa katika ziara mkoani Singida aliweka wazi kuwa yeye anauchukia sana ubinafsishaji na kusema ndiyo umeturudisha nyuma na kuharibu mipango mizuri ambayo alikuwa nayo Mwalimu Nyerere, huku akitolea mfano viwanda kadhaa ambavyo vipo Morogoro na vimeshindwa kuendelezwa na majengo yake kugeuka magodauni ya watu.
==>>Hii ni taarifa ya Ikulu
Social Plugin