MAHAKAMA ya Rufaa imekubaliana na rufaa ya serikali dhidi ya viongozi wa Uamsho akiwamo Julaiarid Hadi Ahmed na wenzake 21, kwamba Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam haikuwa na mamlaka ya kusikiliza masuala yaliyobainishwa na mawakili wa washitakiwa hao.
Kutokana na hali hiyo, mahakama hiyo ya Rufani imefuta mwenendo wa Mahakama Kuu kuhusu maombi ya marejeo yaliyokuwa yamewasilishwa na viongozi hao wa Uamsho na kuelekeza shauri liendelee katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pale lilipofikia kabla ya maombi hayo kupelekwa Mahakama Kuu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Batueli Mmila, Rehema Mkuye na Kipenka Mussa. Jopo hilo lilifikia kutoa hukumu hiyo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili pamoja na sheria zilizoainishwa ambazo ni Kifungu namba 243 na 246 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kwamba hakuna ubishi kuwa mamlaka ya mahakama ya chini yana mipaka.
Jopo hilo limesema mamlaka ya hakimu ni madogo ambayo anaruhusiwa kuamuru hati ya mashitaka kusomwa kwa washitakiwa na kusomwa kwa hati za mashahidi ambapo baadaye wanapeleka shauri hilo mahakama kuu kwa ajili ya kusikilizwa.
Kwa sheria hiyo, hakimu hana kazi nyingine zaidi ya kuruhusu hati kusomwa kwa washitakiwa kwa hivyo, masuala yaliyoainishwa Septemba 3, 2014 yalikuwa ni masuala ambayo mahakama ya Kisutu haikuwa na mamlaka na kwamba yalitakiwa kusubiri kuzungumzwa mara baada ya kupelekwa mahakama Kuu kusikilizwa.
“Tumekubaliana na upande wa mashitaka ukiongozwa na Peter Njika kwamba pale ambapo mahakama ingeona kuna mapungufu kwenye hati ya mashitaka, Hakimu anachopaswa kufanya ni kushauri upande wa mashitaka kuondoa mashauri hayo,” lilisema jopo hilo, na kuongeza kuwa haikuwa sahihi kwa Jaji Dk Fauz Twaibu wa Mahakama Kuu kuleta tafsiri kwa kujumuisha hata makosa yanayosikilizwa na Mahakama Kuu.
Serikali iliwasilisha rufaa hiyo dhidi ya walalamikiwa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa Desemba 19, 2014. Mbali na Ahmed, washitakiwa wengine ni Jamal Swalehe, Nassor Abdallah, Hassan Suleimani, Antari Ahmed, Mohammed Yussuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally, Juma Sadala Juma, Said Ally, Hamis Salum, Said Salum, Aboubakar Mngodo, Salum Ally Salum, Salum Armor Salum, Alawi Amir, Rashid Ali Nyange, Amir Juma, Kassim Nassoro, Said Sharifu, Mselem Mselem na Abdallah All. Julai, 2014, Ahmed na wenzake 21 walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama kutenda kosa, kusajili watu kujihusisha na ugaidi na kuhifadhi watu wanaojihusisha na vitendo vya ugaidi.
IMEANDIKWA NA FRANSISCA EMMANUEL-HABARILEO
Social Plugin