Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU) umeutangazia Umma kuwa kuanzia Julai 22 mwaka huu vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini vitaanza kupokea maombi ya udahili kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Prof. Eleuther Mwageni ameyasema hayo jana, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya kuanza rasmi udahili kwa mwaka 2017/2018.
Prof. Mwageni alisema kuwa waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kwenye vyuo husika na siyo tena TCU kama ilivyokuwa kwa mwaka jana na miaka mingine ya nyuma.
Aidha alisema kuwa waombaji wahakikishe wanaomba programu za masomo ambazo zimeidhinishwa na kutambuliwa na TCU na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
“Tunavikumbusha vyuo kutangaza programu ambazo zimeidhinishwa na kutambuliwa na TCU na NACTE, ikiwa chuo kitatangaza programu ambazo hazitambuliki na Tume, basi chuo husika kitachukuliwa hatua,” alisema Prof. Mwageni.
Aliendelea kwa kusema kuwa, orodha ya programu hizo inapatikana katika tovuti ya TCU ( www.tcu.go.tz) ambapo programu hizo zimegawanywa katika makundi mawili yaani Kidato cha Sita na Diploma.
Vile vile, Prof. Mwageni aliwataka waombaji watakao chaguliwa kwa zaidi ya chuo kimoja, kuthibitisha kwa wakati chuo watakachokwenda ili kutoa nafasi kwa waombaji wengine.
Waombaji wamehimizwa kusoma kwa makini mwongozo wa udahili kwa mwaka 2017/18 ambao unapatikana kwenye tovuti ya Tume.
Aidha Tume inawakaribisha wadau wote kushiriki maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam kuanzia Jula 26 hadi 29 mwaka huu ambapo zaidi ya vyuo 80 vinatarajiwa kuwepo katika maonesho hayo.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO.
Social Plugin