Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hapendi kukamatwa na vyombo vya dola kwa kuwa mahabusu si mahala pazuri pa kuishi watu hususan wasiokuwa na hatia, hata hivyo amesema kitendo hicho hakitamuogofya na kuzuia harakati zake za kupaza sauti.
Lissu ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema kukamatwa na vyombo vya dola, na kuwekwa mahabusu.
“Sipendi kukamatwa mahabusu si pazuri, lakini inafikia hatua inabidi uamue kama kwenda machinjoni ukiwa umenyamaza kimya au kuingia huku unapiga kelele mataifa yasikie,” amesema.
Lissu ambaye mpaka sasa ana kesi za jinai takribani nne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwemo ya uchochezi, amedai kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wako katika hali ya hofu katika utendaji kazi wao, huku akiwataka wananchi kupaza sauti ili hali hiyo iondolewe.
“Hofu kila mahali, mahakamani na hata kwenye utumishi wa umma hakuna aliyeko salama. Viongozi wa dini wako kimya wanadhani wako salama. Tunahitaji kupaza sauti kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.
Social Plugin