WAZIRI MKUU AWAONYA MADIWANI WA KYELA MBEYA KUENDEKEZA MIGOGORO,ATISHIA KUVUNJA BARAZA LA MADIWANI

Serikali imewapa siku mbili Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya kumaliza tofauti zao zinazokwamisha utendaji wa Halmashauri hiyo na kuendelea kufanya kazi walizotumwa na wananchi.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa jana Julai 29, 2017 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Mbeya.

“Baraza la Madiwani limegawanyika,mnamgogoro tunataka uishe na mshirikiane na mshikam ane katika kufanya shughuli za maendeleo ili wananchi waweze kupata manufaa. Mkiendeleza migongano hatutawavumilia Serikali ina uwezo wa kutalivunja baraza.”

Majaliwa amesema ikifika Jumatatu Julai 31, 2017 Madiwani hao wawe wamemaliza tofauti zao na wawaite wakuu wa Idara na kuwapa taarifa hiyo ili shughuli za maendeleo ziendelee kutekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo.

Tofauti hizo ambazo zimedumu kwa takriban mwaka mmoja zimesababisha Madiwani hao kushindwa kufanya vikao jambo linalokwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi katika Halmashauri hiyo.

Amesema baadhi ya Madiwani hao wanawatetea watumishi waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za kuiibia Serikali mabilioni ya fedha jambo ambalo halikubaliki na halivumiliki. “Naombeni mmalize tofauti zenu mara moja kabla sijaondoka.”

Aidha, Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya kuhakikisha watumishi wote waliohusika katika kula fedha za umma wanachukuliwa hatua kama alivyopendekeza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post