Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Kanda ya Kaskazini Kati, Solomoni Masangwa
****
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Kanda ya Kaskazini Kati, Solomoni Masangwa (pichani) amemuonya mbunge wa Siha, Godwin Mollel (Chadema) kuacha kuhubiri siasa chonganishi kanisani kwa kuwatukana viongozi waliopo madarakani na kutoa onyo kwa viongozi wa kanisa hilo kutoruhusu wanasiasa kufanya siasa kanisani.
Kauli hiyo ameitoa juzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa kanisa KKKT dayosisi ya kaskazini kati, jimbo la Arusha Magharibi usharika wa Kiranyi.
Askofu huyo alikerwa na hatua ya mbunge Mollel kujinadi kisiasa huku akimshambulia Rais John Magufuli bila kujali kuwa mkusanyiko uliopo kanisani ni waumini wenye itikadi tofauti za kisiasa na kwamba mahala pale palikuwa sehemu takatifu ya kuabudiwa na siyo jukwaa la siasa.
‘’Napenda kutoa angalizo kuwa kanisani siyo sehemu ya siasa na nisingependa kuona siasa ikihubiriwa kanisani tena,” alisema.
Mbunge huyo wa Siha akiwa kanisani hapo alisema ‘’Kuna mwanaume mmoja hapa Tanzania anajiona yeye ni kidume kuliko wanaume wote ila ajue wapo wanaume zaidi yake sasa”.
Kutokana na kauli hiyo, askofu huyo akasema “Sijui anamlenga nani bila shaka anamaanisha Rais Magufuli, kauli hiyo siyo kauli njema sana na inastahili kukemewa na kila mtu”.
Awali mbunge Mollel alisikika akitamka kanisani hapo kwamba nchi hii imefikia pabaya mwanaume mmoja amekuwa na maamuzi hata kama ni ya kuhatarisha amani na atambue kuwa akijiona yeye ni mwanaume pekee akiongoza lakini ajue wapo wanaume zaidi yake na ipo siku wanaume wengine watavunja ukimya.
IMEANDIKWA NA JOHN MHALA-HABARILEO ARUSHA
Social Plugin