Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefunguka na kusema kuwa wao kama viongozi watamsifu Rais pale anapofanya vizuri hadharani na kusema anapokosea lakini amedai hawawezi kumdhihaki Rais wala kusema mambo ya uongo dhidi yake.
Lema alisema hayo jana katika mkutano wake wa tisa jimboni kwake kwenye Kata ya Sekei Sanawari, Arusha Mjini na kusema anashangazwa na watu ambao wanasema Rais hatakiwi kusemwa hadharani.
"Sitaongea uongo hadharani na sipo hapa kumdhihaki Rais ila Rais akikosea nitamsema na sitamsema chumbani bali nitamsema hadharani, habari ya nchi inavyoendeshwa tunasema hadharani, Rais akikosea tutamsema hadharani na akipatia tutampongeza hadharani" alisema Godbless Lema
Aidha Mbunge Lema aliendelea kutoa lawama zake kwa viongozi mbalimbali wa dini akisema kuwa wamekuwa wakifumbia macho mbalimbali ambayo yanaendelea ndani ya nchi hivyo ameahidi kuwa akimaliza mikutano yake atakuja kufanya mikutano mingine kuhamasisha wanachi wasitoe sadaka kwa taasisi za dini kwa kuwa viongozi hao wamekuwa wakifumbia macho na kushindwa kusema juu ya ukiukwaji wa sheria ndani ya nchi na namna ambavyo Demokrasia imekupwa ikiminywa.
Mbali na hilo Lema alisema anawashangaa watu wanaosema kuwa Mwanasheria wa CHADEMA Tundu Lissu siyo mzalendo kwa kuwa ameweza kusema kuwa kuna ndege ya Tanzania imeshikiliwa nchini Canada.
"Leo Lissu anakamatwa kwa sababu ya kusema ndege ya Tanzania imekamatwa kwa kuwa tunadaiwa Ulaya, Polisi wanamchukua Lissu na kwenda kumsachi kwake, mnatafuta ndege chumbani kwa mke wa Tundu Lissu, wanasema Lissu si mzalendo sasa nani mzalendo aliyesema tunadaiwa Ulaya au aliyetaka kuchukua fedha kinyemela akalipe deni Ulaya" alihoji Godbless Lema
Social Plugin